Ofisa utumishi atuhumiwa rushwa ya ngono

28Feb 2019
Na Mwandishi Wetu
Mkuranga
Nipashe
Ofisa utumishi atuhumiwa rushwa ya ngono

OFISA Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, Valintine Mbai, amedaiwa kutumia nafasi yake kuomba rushwa ya ngono kwa watendaji wa vijiji katika halmashauri hiyo.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mary Mwanjelwa, picha mtandao

Kutokana na tuhuma hizo, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mary Mwanjelwa, amemwonya kuacha tabia hiyo na kubadili mwenendo wake.

Mwanjelwa alitoa onyo hilo juzi wilayani Mkuranga, wakati wa kikao cha kazi na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji, kabla ya kuanza kutembelea wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini katika halmashauri hiyo ili kujiridhisha na utekelezaji wake.

Akizungumza na watumishi hao, Mwanjelwa amesema ni aibu kwa ofisa huyo mwenye dhamana ya kusimamia maadili ya kiutumishi kutumia madaraka yake vibaya kwa kuomba rushwa ya ngono kutoka kwa watendaji wa vijiji jambo ambalo ni kinyume cha maadili ya kiutendaji katika utumishi wa umma.

Amemtaka ofisa huyo kuacha tabia hiyo na kujirekebisha mara moja ili awe mfano bora kwa watumishi anaowasimamia kimaadili.
Pia alimtaka kuwa na heshima kwa wakuu wake wa kazi akiwamo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo ili kutengeneza mazingira mazuri ya kiutendaji.

Aidha, Mwanjelwa alitoa angalizo kwa Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Juma Abeid, kutowatetea watumishi wasio waadilifu na badala yake awachukulie hatua za kinidhamu hata kama ni marafiki zake.

Naibu Waziri alihimiza uwajibikaji kwa watumishi wa umma nchini na kutoa wito kwa watumishi wote kuhakikisha wanazingatia kanuni za maadili ya utendaji kazi katika utumishi wa umma.

Habari Kubwa