Ongezeko la watu linavyotishia  uhai Hifadhi ya Ngorongoro

26Jan 2021
Salome Kitomari
Aliyekuwa NGORONGORO
Nipashe
Ongezeko la watu linavyotishia  uhai Hifadhi ya Ngorongoro
  • *Wafikia zaidi ya asilimia 1,000

ENEO la Hifadhi ya Ngorongoro lililoanza mwaka 1959 likiwa na watu 8,000, sasa limeelemewa kwa idadi kubwa ya watu zaidi ya 100,000, huku kukiwa na ongezeko la mifugo kiasi cha kutishia uhai wao.

Moja ya vijiji katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), eneo ambalo lina ongezeko la watu na mifugo kiasi cha kushindwa kuwa na uwiano wa uhifadhi na shughuli za kibinadamu. PICHA: SALOME KITOMARI, NGORONGORO

Ngorongoro ilianza baada ya kumegwa kutoka eneo la Serengeti Game Reserve na kuunda Hifadhi ya Taifa ya Serengeti iliyo chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), baada ya watu 4,000 kuhamishiwa ndani ya Ngorongoro na kuanza uhifadhi na makazi.

“Najaribu kuitazama Ngorongoro miaka 10 ijayo kwamba itakuwa katika hali gani kama kasi ya watu itakuwa hii, shughuli za uhifadhi zitakuwa ngumu, migogoro baina ya jamii na wanyama itaongezeka, tutawezaje kwenda pamoja na maendeleo endelevu ya binadamu na uhifadhi,” Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Dk. Freddy Manongi, anaeleza hofu yake.

Mathalani, anasema hivi karibuni diwani mmoja alinitumia picha ya fisi aliyevamia boma na kuua kondoo 38, wananchi walipiga simu wakiomba msaada tuzuie, mambo kama hayo kujitokeza ambayo ni ngumu kuzuia kitaalamu, jambo ambalo linaonyesha kila shughuli sasa inasababisha migogoro baina ya pande mbili.

Anasema kamisheni iliyoundwa na wizara kuangalia sera ya matumizi mseto ya eneo la Ngorongoro na timu ilihoji watu wengi na kushirikisha wadau kutaka kujua hatima ya eneo hilo ambalo kwa sasa linachangamoto nyingi.

 

“Balance (uwiano) kati ya uhifadhi wa wanyamapori, malikale na maendeleo ya binadamu ndani ya hifadhi imefikia mahali pagumu sana, kila unachofanya kwa maana ya uhifadhi kina athari kwa maisha ya binadamu wanaoishi ndani ya hifadhi na kila ruhusa au fursa unayoitoa kwa wenyeji inaathari hasi kwa uhifadhi,” anasema na kuongeza;

 

“Hiyo tume imeona hali hiyo wazi na kumekuwa na malalamiko mengi kwa wahifadhi kuhusu idadi ya watu, lakini uharibifu unaotokana na uhifadhi, kumekuwa na malalamiko mengi kwa jamii kuwa shughuli za uhifadhi zinawaumiza,” anabainisha.

Kwa mujibu wa Dk. Manongi, Tume ilimaliza kazi Mei mwaka huu, na kuwasilisha ripoti kwa Waziri wa Maliasili na kubwa waliloshauri ni eneo hilo kugawanywa katika kanda na kila moja iwe na idadi ya shughuli za uhifadhi na kibinadamu zinazofanyika kama suluhisho.

“Hii itasaidia kutenga maisha ya binadamu na maisha ya wanyamapori, itawapata fursa kwa wenyeji kuendelea na shughuli zao kama kawaida huku uhifadhi, pia ukiendelea bila kuwa na mgongano baina ya pande mbili,” anasema.

Akiwasilisha mada ya ‘ilikotoka, ilipo na inakokwenda Ngorongoro’, Ofisa Mwandamizi wa Uhifadhi, Dk. Elibariki Bajuta, anasema majukumu ya kisheria ya Ngorongoro ni kuendeleza uhifadhi na utalii, wenyeji waliopo ndani ya hifadhi na kwamba kidunia ni muhimu sana.

“Tukishindwa kubalance (uwiano) wa matumizi ya eneo hili ndiyo tutashindwa kufikia malengo husika,” anasema.

 

ONGEZEKO LA MIFUGO NA WATU

Anasema Ngorongoro ilifanya sensa kujua idadi ya mifugo, watu na makazi ndani ya eneo, ili kupanga matumizi na kuona mfumo wa matumizi ya eneo hilo kwa ushirikiano.

Kwa mujibu wa Dk. Bajuta, pamoja na mafanikio makubwa kuna tatizo kubwa la ongezeko la watu ambalo siyo wa kuzaliana bali walioingia ndani ya hifadhi.

“Miaka ya 90 aliyekuwa Waziri Mkuu, John Malecela, aliruhusu kilimo cha kujikimu ambacho kilileta watu wengi sana ndani ya hifadhi, tangu kuanza kwa hifadhi mwaka 1959 kuna ongezeko la watu zaidi ya asilimia 1,000, hii si hali nzuri kwa utalii na uhifadhi,” anasema.

“Mifugo nayo imeongezeka kwa kiasi kikubwa mno na asilimia 20 wanamiliki asilimia 80 ya mifugo iliyopo na kubwa zaidi kuna ongezeko kubwa la magonjwa kutoka kwa wanyamapori kwenda kwa wanyama wanaofugwa na kutoka kwa wanyama wanaofugwa kwenda kwa wanyamapori, hadi kwa wenyeji na kuleta balaa,” anasema.

“Magonjwa haya hata tiba yake ni shida sana maana jamii maisha wanayoishi siyo mazuri sana,” anasema.

 

UHARIBIFU WA MAZINGIRA

Dk. Bajuta anasema kasi ya uharibifu wa mazingira ni kubwa kutokana na ongezeko la watu na mifugo pamoja na wanyamapori, ushindani katika utekelezaji wa majukumu ya uhifadhi, utalii na maendeleo ya watu ni changamoto.

Anasema kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na sababu nyingi kama kuongezeka kwa watu na wanyama wanaofugwa vyanzo vya maji vimepotea na kupungua kwa huduma hiyo muhimu hifadhini.

“Kubwa zaidi ni kuongezeka kwa migogoro baina ya wanyamapori na binadamu, mfano fisi kaua kondoo 38, kuna kaya zaidi ya 20,000, tuna askari pungufu 300, huwezi kulinda kila kaya na mifugo, haya yote yapo nje ya hifadhi ila ndani ya hifadhi ni ngumu sana,” anasema na kuongeza:

Nje ya hifadhi tembo wanakula mazao ya wananchi na kwa sheria ya wanyamapori mamlaka hairuhusiwi kutoa kifuta machozi kwa sababu tayari tunaishi na wanyamapori.

MAGUGU VAMIZI

“Makazi yameongezeka sana kwa sababu watu wameongezeka, bado tunajitahidi kubana kuhakikisha hawajengi bila vibali, lakini bado changamoto ni kubwa sana na kutokana na kuongezeka kwa watu na mifugo sasa hifadhi imepata magugu vamizi,” anasema.

Kwa mujibu wa Bajuta, ndani ya eneo la kreta, asilimia 70 ya eneo limepata magugu vamizi kutokana na mifugo na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu.

Aidha, anasema umaskini ndani ya hifadhi ni mkubwa unaosababishwa na sheria inayosimamia eneo hilo kwa kuwa wananchi hawaruhusiwi kufanya shughuli nyingine yoyote ya kujipatia kipato zaidi ya ufugaji na wengi hawana mifugo.

UMASKINI/ KIWANGO CHA UJINGA

“Umaskini ni mkubwa sana ndani ya hifadhi kwamba hata mtu kumudu milo mitatu kwa siku ni ngumu sana, na ndiyo maana serikali iliamua hakuna kuwapa chakula,” anasema.

Anasema sensa ya mwaka 2017 iliyofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ilionyesha kuwa asilimia 64.5 ya wananchi hawajui kusoma na kuandika, huku kukiwa na shule 25 za msingi na mbili za sekondari.

 

HATUA ZILIZOCHUKULIWA

Anasema Ngorongoro imefikia mahali wakijibana katika kusaidia jamii wanaumiza uhifadhi na wakijibana katika kulinda wananchi wanaumiza uhifadhi na ndiyo maana wamekuja na mipango mbalimbali.

Mipango hiyo ni ya kupambana na magugu vamizi inayotekelezwa chini ya Ofisi Makamu wa Rais, mwingine ni kuhakikisha utalii endelevu ndani ya hifadhi kwa kuwa kipindi cha juu cha utalii kuna magari 700 ndani ya kreta, kuboresha miradi ya maendeleo na kuboresha mifugo ili kuachana na idadi kubwa ya mifugo, hifadhi na mifugo viwepo.

“Kuna mambo hayapo ndani ya uwezo wetu kama kupitia upya muundo wa eneo la Ngorongoro, kamati imeshafanyakazi yake na kuwasilisha wizarani tunasubiri matokeo,” anasema.

Pia wanafanya mapitio ya mpango mkuu wa Ngorongoro unaotarajia kukamilika hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya sheria iliyounda eneo hilo ambayo yalifanyika mara ya mwisho mwaka 2002, itayokuja na hali halisi ya hifadhi na hatua za kuchukua.

 

WAJIBU WA NGORONGORO KWA JAMII

Anasema Baraza la Wafugaji lilianzishwa mwaka 2000 likiwa na wajibu wa kuibua miradi ya jamii kwenye hifadhi, huku wajibu mkubwa wa Ngorongoro ukiwa ni kuwaendeleza kielimu, kiafya, maji na mifugo yao ambayo ndiyo kazi yao kubwa.

Baraza hilo pia, lina wajibu wa kusimamia miradi ya elimu kwa kuwa wanapewa fedha za kusomesha wanafunzi na anaamini akielimika anaenda Arusha kuliko wakiwaacha ndani ya hifadhi na kwa kufanya hivyo wanapunguza idadi ya watu.

Dk. Bajuta anasema pia wanasaidia kuhakikisha miradi inatunzwa, kuwa na mawasiliano baina ya jamii na mamlaka.

UPEKEE WA NGORONGORO

“Ni eneo dogo lililopewa hadhi tatu kidunia, ya kwanza ilitolewa pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti mwaka 1979 kuwa ni eneo la urithi wa duniani kutokana na baonuwai iliyopo, maliasili na vivutio vilivyopo, mwaka 2010 ilitambuliwa kama eneo la urithi mchanganyiko ambalo unaweza kupata taarifa mbalimbali mfano eneo la Oldvai George ambalo ni pekee duniani, unaweza kupata historia ya binadamu wa kale,” anafafanua.

“Kuna eneo la Laitol ndiyo pekee duniani lenye ushahidi kuonyesha binadamu alianza kutembea na miguu miwili na ndiko kuna ushahidi wa nyayo, pamoja na maeneo ya uhifadhi na jamii kwa ujumla,” anasema.

Hadhi nyingine anasema, ilitolewa mwaka 2018 ikitambulika kama eneo la utalii wa miamba na sura za nchi Geopark, eneo pekee Kusini mwa Jangwa la Sahara na ya kwanza nchini, ikisababishwa na maeneo yaliyoko ndani ya hifadhi na pembezoni kama Mlima Oldonyo Lengai na mchanga unaohama kwa takribani mita 17 kwa mwaka.

Maeneo mengine ya Geopark ni miinuko na mabonde kama kreta ya Ngorongoro, Almoti, Embakai na maeneo ya maji moto ya Easi na Engaruka.

“Hadhi hizi tatu zimeifanya Ngorongoro kuwa muhimu kidunia, ni eneo UNESCO kulipa hadhi tatu inaonyesha umuhimu wa Ngorongoro kitaifa na kimataifa,” anasema.

“Lengo kuu la Ngorongoro ni kuhakikisha majukumu ya uhifadhi, utalii na kuendeleza wananchi waliomo yanawekwa katika usawa, bila hivyo eneo hilo litabaki historia,” anasema.

MUUNDO WA NGORONGORO

Dk. Bajuta anasema mfumo wa usimamizi wa eneo hilo uko chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii, ambayo kuna Waziri, Katibu Mkuu na Bodi pamoja na Kamishna wa Hifadhi na wasaidizi wawili na kote kuna idara zilizo chini yao na kubwa ni Kurugenzi ya Maendeleo ya Jamii na Utalii.

Anasema Ngorongoro imepata mafanikio makubwa ya uhifadhi na utalii ambayo ni juhudi za serikali kuhakikisha inaendelea kuwapo.

MAPATO

“Mapato yameongezeka kwa kiwango kikubwa 2014/15 walikusanya Sh. bilioni 60 na mwaka 2018/19 walikusanya Sh. bilioni 143, huku mwaka 2019/20, licha ya corona walikusanya Sh. bilioni 122, ni mafanikio makubwa sana tuliyoyapata,” anasema.

Aidha, anasema kuongezeka kwa mapato kuna maana kubwa katika kuchangia pato la taifa na imekuwa ni kati ya taasisi tano bora za serikali zinazotoa gawio kwa serikali na mwaka 2017/18 walichangia Sh. bilioni 18 ambayo ni asilimia 15.

Anasema mwaka 2018/19 walitoa gawio la Sh. bilioni 23 ikiwa ni mafanikio makubwa, na kwamba mwaka 2019/20 pamoja na corona walitoa gawio la Sh. bilioni 15.

Kwa upande wa utalii, pamoja na mapato kuongezeka idadi ya wageni haikuwa nzuri na sababu kubwa ni mifumo thabiti ya ukusanyaji mapato na juhudi za mamlaka kukusanya mapato.

Anasema kuanzia mwezi Machi hadi Aprili, 2020 hakukua na mgeni hata mmoja kutokana na janga la corona na hawakukusanya fedha yoyote bali walitumia muda huo kuboresha miundombinu ya barabara, majengo na uatlii kwa ujumla.

“Tumejenga jengo la kitega uchumi jijini Arusha ambalo linasaidia watalii kupata taarifa mbalimbali, huku wakiboresha mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato, uendeshaji wa shirika na bajeti,” anasema.

Habari Kubwa