Ongezeko la watu, mifugo tishio

17Jun 2019
Salome Kitomari
ARUSHA
Nipashe
Ongezeko la watu, mifugo tishio

ONGEZEKO la watu na mifugo kwenye Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), limekuwa tishio kwa binadamu, mifugo na wanyamapori.

Tangu mwaka 1959 watu waliokuwa wanaishi kwenye eneo la Serengeti waliondolewa na kupelekwa Ngorongoro ambako kumeruhusiwa wanyama wafugwao, wanyamapori na binadamu kuishi pamoja.

 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi wanaoishi ndani ya hifadhi katika eneo la Seneto, maarufu kama Masai Boma, walisema ongezeko hilo ni tishio kwa pande zote.

Viongozi hao waliongea na waandishi wa habari 10 wa Tanzania na Thailand, walio kwenye programu maalum ya kuandika habari za ujangili na uhifadhi, iliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET), kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID).

Viongozi wa eneo hilo Mwenyekiti wa Vijana, Tunai Kasyaro na Mwenyekiti wa Boma, Bahati Miando, walisema mwaka jana maelfu ya mifugo ilikufa kutokana na ukame.

"Mtu alikuwa na ng’ombe 400 walikufa wote kutokana na ukame, raha ya Masai ni kuona mifugo mingi na inapokufa anabaki kuwa maskini, inatuumiza sana kichwa," alisema Miando.

Alisema eneo hilo lenye maboma saba lina watu 120 na kwamba wanajitahidi kuzuia wageni ili kupunguza ongezeko la watu kutokana na eneo kuwa ni lile lile.

Viongozi hao walisema kwa sasa wanafikiria uwezekano wa kupunguza mifugo na kufuga michache yenye tija, kwa kuwa wanaona hasara ya mifugo mingi ambayo inakosa sehemu za malisho.

"Masai na mifugo ni pete na kidole, ni raha sana sisi kuwa na mifugo, lakini mabadiliko ya hali ya hewa na ongezeko la watu ni tishio kwetu kwa kuwa sasa ardhi haitoshi nasi tunaongezeka, huku ukame ukishika kasi," alisema Kasyaro.

Aidha, alisema pia wanatamani kuishi kwenye nyumba nzuri na kuondokana na wanazoishi sasa ambazo nyakati za mvua maji huingia ndani na maisha kuwa magumu zaidi.

Walisema kwa sasa wanauza mifugo ili wanunue chakula kingine kwa kuwa nyakati za kutegemea nyama na maziwa zimebadilika na sasa wanakula vyakula vingine.

Aliishukuru NCAA kwa kuwapa elimu, kujenga shule za msingi na sekondari zikiwamo za bweni ambazo zimewezesha watoto wao kupata elimu.

Hivi karibuni, Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA, Dk. Freddy Manonga, alisema kiwango cha watoto wasiojua kusoma na kuandika ni asilimia 64 na kwamba hadi sasa haijulikani sababu ni nini kwa kuwa kuna shule zenye miundombinu mizuri.

Alisema idadi ya mifugo inayokufa kutokana na ukame, magonjwa ya kimeta na kichaa cha mbwa inaongezeka, huku binadamu wanaoliwa na wanyama au kupata magonjwa ya wanyama na mifugo kupata magonjwa ya wanyamapori inaongezeka.

"Mamlaka inapata fedha nyingi sana kutokana na utalii, lakini hazifanani na maisha ya watu wa eneo husika. Tunapata wastani wa Sh. bilioni 120 kwa mwaka na watalii 600,000, lakini bado watu wetu ni maskini sana, tunawapa fedha kupitia baraza lao, lakini bado maisha yao ni yale yale," alibainisha.

Habari Kubwa