Onyo wahalifu walioachiwa kwa msamaha wa Rais

17Jan 2018
Beatrice Shayo
Nipashe
Onyo wahalifu walioachiwa kwa msamaha wa Rais

JESHI la Polisi limewaonya watu waliopata msamaha wa Rais kuwa iwapo watarudia kufanya vitendo vya uhalifu, watachukuliwa hatua ikiwamo kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

 Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana,  Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema taarifa za kiintelijensia zinaonyesha kuwa baadhi ya waliotoka gerezani kwa msamaha wa Rais  wanatumwa na wenzao ambao wako jela na kuwaelekeza waende sehemu fulani kuchukua silaha na watakapozifanyia kazi wawapelekee posho jela.

Alisema askari waliweka mtego na kufika eneo la nyumbani kwa mzee Said Omary (62) na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili wakiwa na silaha  aina ya AK 47 yenye namba UC 49331998 ambayo haikuwa na magazine yake.

Mambosasa aliwataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni Ally Makwaya (40) na Fredrick Odhiambo (50), wote wakazi wa Tandale kwa Tumbo.

Alisema walipohojiwa  kuhusu wapi waliipata silaha hiyo, walieleza kuwa shughuli zao kubwa ni kuokota makopo na vyuma chakavu na kuwa hata silaha hiyo waliiokota kwenye karakana ya magari (gereji) Kinondoni Mwinyijuma.

Aidha, alisema watuhumiwa hao walieleza kuwa baada ya kuikota silaha hiyo hawakutoa taarifa katika kituo chochote cha polisi, hivyo waliamua kutafuta mteja wamuuzie, ili kupata pesa za kujikimu.

 Alisema silaha waliyoikamata ya AK 47 ni silaha kubwa na ni toleo la mwanzo na wahusika wakati wanajitetea walisema wameitoa kwenye vyuma chakavu kwa vile tu imekutwa na kutu.

“Kwa taarifa zetu za kiintelejensia tulizo nazo ni kwamba silaha hii ni moja ya zilizofukiwa na wahalifu, lakini wakasingizia kuwa ni chuma chakavu kwa kuwa ina kutu. Taarifa tulizo nazo ni kwamba baadhi ya waliokuwa wafungwa na kuachiwa kwa msamaha wa Rais, wanahusika na vitendo kama hivi na wamekwenda kufichua silaha ambazo walizifukia ardhini na sasa wanaziibua kwa ajili ya kuzitumia,” alisema Mambosasa.

Kutokana na taarifa hizo, Mambosasa alionya kuwa mtu yoyote ambaye amepata msamaha badala ya kumshukuru Mungu na kubadili tabia, halafu anaanza  kufukua silaha kwa ajili ya kuendeleza vitendo vya kihalifu, hatabaki salama.

“Tutawaandalia mashtaka na kuwarudisha huko walikotoka. Ukipata msamaha kitu cha kwanza ni kumshukuru Mungu na kuachana na uhalifu. Hii bunduki ni kwamba imefukuliwa chini na si  kwamba imekutwa kwenye vyuma chakavu kama wanavyodai washtakiwa hao. 

“Hawa ni waongo na wako wengine wanashirikiana na walioko jela wanawatuma walipoficha silaha wanaenda kuzichukua na kuanza kuingia nazo mtaani, tuko imara tutawakamata,” alisema Mambosasa.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limesema limepokea taarifa za mchungaji kudaiwa kufanya utapeli na kwamba jambo hilo wanalifanyia kazi ili haki ipatikane. 

“Hili shauri sitaki kulizungumzia sana kwa kuwa linachunguzwa na wakubwa zangu, lakini nasema kutokana na hilo kuna uhalifu mwingine umetendeka kwa kutumia hati iliyoghushiwa. Hilo limeripotiwa rasmi leo (jana) na huyo mama  yupo juu (kituo kikuu cha polisi) anaandika maelezo,” alisema.

“Akishakamilisha huyu mhusika ambaye ni mchungaji, lakini bado sijaamini kama ni mchungaji, sijui anachunga binadamu au mbuzi maana mchungaji siwezi kuamini kama anaweza kuyatenda hayo aliyoyafanya.

“Ni kweli amefanya vitendo vya machukizo makubwa, ameghushi hizo ‘documents’ (nyaraka) na kusababisha  mama kupoteza nyumba Kariakoo, Mikocheni na kiwanja kilichoko Bahari Beach. Kwa hiyo huyo si mchungaji ni muuaji  maana katika tukio hilo mume wa huyo mama amepooza.”  

Habari Kubwa