Operesheni ya DC Sabaya yanasa lita 4,800 za gongo Hai

05Sep 2019
Godfrey Mushi
MOSHI
Nipashe
Operesheni ya DC Sabaya yanasa lita 4,800 za gongo Hai

OPERESHENI ya siri inayoongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro Lengai Ole Sabaya ya kuwabaini wafanyabiashara sugu wanaotengeneza na kusambaza pombe haramu ya gongo, imenasa lita 4,800 na mitambo sita katika kiwanda kidogo kilichojitenga na makazi ya watu.

Leo, Ole Sabaya alikwenda kimya kimya katika Kijiji cha Mtakuja, Kata ya Kia, bila ya kuwa na askari wa Jeshi la Polisi na kuwanasa watu wanne ambao ni wamiliki wa mitambo hiyo.

“Ni kweli mimi nimekwenda mwenyewe Kijiji cha Mtakuja na nimewakamata hao watu na kuita Polisi wakaja kuwachukua. Nilikuta kiwanda kimoja kina lita 4,800 za pombe hiyo, mapipa 42 na mitambo sita ya kuzalisha gongo,”amesema

Amesema mbali na wafanyabiashara hao wanne, pia ameagiza uongozi wa serikali ya Kijiji cha Mtakuja na Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kia, kuwapelekea taarifa ya wito ya kujisalimisha katika ofisi yake ndani ya saa 72.

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya (aliyevaa shati la blue) akiwa amebeba moja kati ya mapipa 42 ya kutengeneza pombe ya gongo yaliyokamatwa katika kiwanda kidogo kilichopo Kijiji cha Mtakuja, Kata ya Kia. PICHA: GODFREY MUSHI

Baada ya kufanikiwa kuwanasa wafanyabiashara hao waliokuwa wakidhani ni mteja, Mkuu huyo wa Wilaya alipiga simu kwa Mkuu wa Polisi wa Wilaya hiyo, Lwelwe Mpina na kufika eneo hilo akiwa na askari katika magari matatu na kuchukua miundombinu yote pamoja na watuhumiwa hao.

Akiwa katika kijiji hicho, Ole Sabaya aliagiza Polisi kufanya mahojiano na watuhumiwa hao wanne ili kuweza kubaini wenzao wanaoshirikiana nao katika biashara hiyo haramu ya gongo na uchunguzi ukikamilika wapelekwe mahakamani.

Ulevi wa kupindukia, unazitesa baadhi ya kaya katika Wilaya ya Hai hasa vijiji vya pembezoni vilivyoko katika ukanda wa tambarare kutokana na kuendelea kukithiri kwa unywaji na uuzwaji wa pombe ya moshi maarufu kama gongo.

Ziko taarifa kwamba wako pia, baadhi ya wanafunzi wamejiingiza katika unywaji wa pombe hiyo, kitu ambacho kinaelezwa kumtia hasira Mkuu huyo wa Wilaya.

Aidha, Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini, Leonard Minja, nae amezungumzia kadhia hiyo akisema taifa linapoteza vijana wanaotegemewa kukuza uchumi kutokana na watu ambao hawana nia njema ambao wamekuwa wakifanya biashara ya gongo.

Mchungaji Minja, amesema kutokana na serikali kuwa na mkono mrefu, anaunga mkono mkakati huo wa kudhibiti pombe hiyo, huku akiitaka serikali isifanye operesheni hiyo kuwa moto wa kifuu.

Habari Kubwa