Osha yaagiza kampuni usafi kuwalinda wafanyakazi

09Mar 2019
Gwamaka Alipipi
Dar es Salaam
Nipashe
Osha yaagiza kampuni usafi kuwalinda wafanyakazi

WAKALA wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha), umewataka wamiliki wa kampuni za usafi nchini kuwalinda wafanyakazi wao kwa kuwapa vifaa kinga pamoja na kuwapa elimu ya kujikinga na afya mara kwa mara.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Osha, Khadija Mwenda, picha mtandao

Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Osha, Khadija Mwenda, wakati akifungua mafunzo kwa wafanyakazi zaidi ya 100 wanaofanya kazi katika sekta ya usafi nchini na wamiliki wa kampuni zinazojihusisha na usimamizi wa usafi wa mazingira.

“Sheria ya afya na usalama mahali pa kazi ya 2003, inamtaka mwajiri aweke mazingira yenye kuzingatia afya, usalama na ustawi kwa wafanyakazi wake wote, hivyo wanapaswa kuwapeleka kupata elimu ya kujikinga pamoja na kuwapatia vifaa kinga,” alisema Mwenda.

Alisema kupitia mafunzo hayo, wafanyakazi wa usafi wa mazingira watapata elimu ya namna bora ya kujikinga wanapokuwa sehemu zao za kazi, pia watapewa vifaa maalumu watakavyovitumia wakiwa kazini.

Alisema Osha imeshawafikia makundi mbalimbali kuwapa elimu ya kujikinga na afya wakiwa sehemu za kazi na kwamba kwa sasa lengo ni kuwafikia walengwa wote katika Jiji la Dar es Salaam.

“Kila robo ya mwaka tutakuwa tunatoa mafunzo, yatakuwa endelevu kwasababu jukumu letu ni kuhakikisha usalama wa kazi kwa Watanzania unazingatiwa,” alisema Mweda.

Mmoja wa wafanyakazi kwenye mafunzo hayo, Rehema Ambali, alisema changamoto kubwa wanayoipata wanapokuwa kazini ni kugongwa na magari, hivyo aliiomba serikali kuwapatia bima pamoja na kuwapima afya kila wakati.

Alisema wafanyakazi wanaofagia katika barabara wengi wao wanaugua magonjwa ya kifua kikuu pamoja na mafua kutokana na kutotumia vifaa vya kujikinga na vumbi.

Naye Meneja Rasilimali Watu wa Kampuni ya Green Waste, Amina Mchomvu, alisema wanawapatia vifaa vya kujikinga wafanyakazi wao, lakini wengi wao hawavitumii kwa madai kuwa vinawazuia kufanya kazi vizuri.

“Wafanyakazi wengine ukiwapa gloves wanasema joto kali, ukiwapa mabuti wanasema wanashindwa kutembea, hivyo tunajitahidi kuwapa elimu ya kutumia vifaa hivyo,” alisema Mchomvu.

Alisema kila kampuni ya usafi nchini inawajibu wa kuwalinda wafanyakazi wake kwa kuwa kwa kufanya hivyo watakuwa wamesaidia kupunguza vifo vitokanavyo na magonjwa ya kuambukiza.

Habari Kubwa