OSHA yawanoa wafanyakazi wa kiwanda cha nondo

09May 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
OSHA yawanoa wafanyakazi wa kiwanda cha nondo

WAKALA wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) imetoa mafunzo maalum ya usalama na afya kwa wafanyakazi wa kiwanda cha kuzalisha nondo cha PNP Industries Limited kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kujilinda dhidi ya ajali na magojwa yanayotokana na mazingira yao ya kazi.

Mwezeshaji wa mafunzo ya usalama na afya kutoka OSHA, Respicious Kundawa , akizungumza na mmoja ya washiriki wa mafunzo hayo.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliofanyika katika kiwanda hicho kilichopo Mikocheni, mkoani Dar es Salaam, Mwezeshaji wa Mafunzo hayo kutoka OSHA, Respicious Kundawa, amesema mafunzo hayo ni muhimu hususan kwa wafanyakazi wanaohusika moja kwa moja katika mchakato mzima wa uzalishaji wa bidhaa hiyo muhimu.

“Katika mafunzo ya leo tumewalenga wafanyakazi katika viwanda vya kuzalisha nondo ambao tunafahamu wanakabiliwa na vihatarishi mbali mbali katika mlolongo mzima wa uzalishaji wa bidhaa husika kuanzia wanapopokea vyuma chakavu, kuvichambua, kuviyeyusha, kutengeneza nondo zenyewe na hata kuzipakia katika magari tayari kwa kuzisafirisha kwenda kutumika,” amesema Kundawa.

Ameongeza kuwa; “Katika hatua zote hizo mfanyakazi anaweza kuumia hivyo ni muhimu kuwapa wafanyakazi nyenzo za kujilinda.”

Mwezeshaji wa mafunzo ya usalama na afya kutoka OSHA, Respicious Kundawa , akitoa mafunzo kwa wafanyakazi wa kiwanda cha PNP Industries Limited.

Kwa upande wa uongozi wa kiwanda hicho umeeleza kuridhishwa na mafunzo yaliyotolewa na OSHA na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yaliyotolewa kupitia mafunzo hayo. 

“Tunashukuru OSHA kwa mafunzo waliyotupatia kwa siku ya leo ambayo yatatusaidia sana katika kuboresha mazingira yetu ya kazi pamoja na namna ambavyo tunafanya kazi,” amesema Iddy Hamis, Afisa Rasilimali Watu wa kiwanda hicho.

Juma Kajembe, mmoja wa wafanyakazi katika kiwanda hicho, amesema mafunzo waliyoyapata yatasaidia katika kuboresha namna ambavyo wamekuwa wakitekeleza majukumu yao na hivyo kujiepusha na ajali na magonjwa yatokanayo na kazi. 

Wafanyakazi wa kiwanda cha PNP Industries Limited wakifuatilia mafunzo ya usalama na afya yaliyotolewa na OSHA kiwandani hapo. Mafunzo hayo yalilenga kuwawezesha wafanyakazi kujilinda dhidi ya vihatarishi wanapokuwa kazini.

“Tunashukuru kwa mafunzo tuliyoyapata kwa siku ya leo, tunaimani yatatutoa kutoka hatua moja kwenda nyingine kahusiana na usalama wetu tuwapo kazini. Kwasasa tunaweza kutambua vitu gana ni hatarishi katika maeneo yetu kazini pamoja na matumizi sahihi ya vitendea kazi na vifaa kinga,” amesema Solomon Lukas ambaye pia ni mfanyakazi katika kiwanda hicho.

Wakati huo huo, OSHA imehitimisha darasa la mafunzo ya usalama na afya katika sekta ya mafuta na gesi yaliyofanyika katika ofisi za OSHA ambayo yalijikita katika kuwaandaa wataalam ambao watatumika kusimamia usalama wa wafanyakazi katika miradi ya mafuta na gesi inayotarajiwa kuanza kutekelezwa hapa nchini.

Mwezeshaji wa mafunzo ya usalama na afya kutoka OSHA, Respicious Kundawa , akitoa maelekezo kuhusu kuboresha mazingira ya kazi kwa wasimamizi wa wafanyakazi wa kiwanda cha PNP Industries Limited mara baada ya kutoa mafunzo ya usalama na afya kiwandani hapo.

Habari Kubwa