Othman Masoud amrithi Maalim Seif

02Mar 2021
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Othman Masoud amrithi Maalim Seif

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amemteua Othman Masoud Othman Sharif, kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Katika taarifa ya vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Zena Ahmed Said, ilisema kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 9(3) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, kinachosema kwamba “Muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utakuwa wa Umoja wa Kitaifa na utendaji wa kazi zake utafanywa katika utaratibu utakaohakikisha kuendelezwa kwa umoja nchini na lengo la kufikia demokrasia.”

Othman anachukua nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad aliyefariki dunia Februari 17, mwaka huu.

Kwa mujibu wa uwezo aliopewa chini ya kifungu namba 39(3) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, baada ya kushauriana na Chama cha ACT-Wazalendo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Mwinyi amemteua Othman Masoud Sharif kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Sharif alikuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kipindi cha miaka mitano ya uongozi wa awamu ya kwanza ya Rais Dk. Ali Mohamed Shein.

Sherehe ya kuapishwa kwa Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar zitafanyika leo Machi 2, 2021 saa 4:00 asubuhi katika ukumbi wa Ikulu, Zanzibar.

Kabla ya uteuzi mpya Othman alikuwa mshauri wa masuala mbalimbali kutoka katika Chama cha CUF na baadaye alipohamia ACT-Wazalendo ikiwamo sheria baada ya uteuzi wake wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ulipotenguliwa na Rais mstaafu Dk. Shein mwaka 2014.

Othman ni msomi wa masuala ya sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo kikuu cha Turin nchini Italia.

Ni mwanzilishi wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP), kufuatia maridhiano ya kisiasa ya muafaka katika kipindi cha Rais mstaafu Amani Abeid Karume na kuendelea na nafasi hiyo katika kipindi cha Rais mstaafu Dk. Shein na kupanda hadi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mapema mwaka 2010.

Uteuzi wa Othman ulitenguliwa mwaka 2014 baada ya kupinga rasimu iliyopendekezwa na Bunge la Katiba.

APONGEZWA

Baadhi ya viongozi wakiwamo wanasiasa na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamepongeza uteuzi huo na kusema ni sahihi kutokana na uwezo wake mkubwa katika masuala ya sheria na uongozi.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi, Kheri Jemes, alisema wanapongeza uteuzi huo na wapo tayari kumpa ushirikiano ili kutekeleza majukumu yake na kuendeleza maridhiano ya kisiasa Zanzibar.

Alisema hawana mashaka kuwa atakuwa msaada kwa Rais Dk. Mwinyi, Wazanzibari wote na atamuezi Maalim Seif Sharif Hamad kama kiongozi alieweka umoja na mshikamano.

Aliwataka vijana wote kushirikiana katika kujenga umoja na mshikamano ili kuchochea shughuli za maeneo na uzalishaji mali, kujenga taswira ya amani, usalama na kivutio cha kweli cha nchi na kuwapa kichocheo cha fikra utendaji bora watendaji wa serikali katika kusimamia malengo yao.

“Kuendelea kuenzi umoja na mshikamano kama silaha ya mwanzo ya kuleta maendeleo kwa wananchi na taifa letu,” alisema.

Alisema vijana wa Chama Cha Mapinduzi lazima wawe na dira ya kusisitiza, kuhimiza, kushikilia na kusimamia misingi ya umoja na mshikamano katika kusimamia misingi ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha ADA-Tadea na mwakilishi wa kuteuliwa na Rais, Juma Ali Khatib, alisema anamfahamu vizuri Othman wakati walipokuwa pamoja katika Bunge la Katiba akionyesha umahiri mkubwa katika masuala ya sheria na katiba.

Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Zanzibar, Othman Makungu ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Mwanasheria Mkuu wa serikali katika kipindi cha Rais mstaafu Dk. Shein, alisema anamfahamu vizuri kwa sababu alimpokea katika taaluma ya sheria katika utumishi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika miaka ya 1989.

Makungu alisema Othman ameteuliwa katika wadhifa ambao anastahiki kwa sababu anakuwa mshauri mkuu wa rais kazi ambayo ameifanya kwa muda mrefu akiwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali hadi kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Sheria katika kipindi cha utawala wa Rais mstaafu Dk. Salmin Amour.

Mwakilishi wa Jimbo la Mfenesini kwa tiketi ya CCM, Machano Othman Said, alisema uwezo wa Othman unafahamika katika kipindi alichofanya kazi akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali pia akiwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi kwa kusaidia marekebisho mengi ya kisheria.

“Mimi nimekuwa mwakilishi kwa muda wa miaka kumi na tano sasa nilikuwa naye Othman wakati huo akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Baraza la Wawakilishi, uwezo wake ni mkubwa katika masuala ya sheria...matarajio yangu makubwa atasaidia na kufanya kazi vizuri na Rais Dk. Mwinyi,” alisema Machano.

Habari Kubwa