Pablo amchambua Bocco

19Jan 2022
Saada Akida
Dar es Salaam
Nipashe
Pablo amchambua Bocco
  • ***Afunguka mazito huku akiwataka mashabiki kuvuta subira, mwenyewe asema...

WAKATI mashabiki wa Simba wakihoji kuhusu uwezo wa mshambuliaji wao, John Bocco, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Pablo Franco, amemkingia kifua na kudai ni suala la muda tu kabla ya mfungaji bora huyo wa msimu uliopita kurejea katika ubora wake.

Bocco, ambaye msimu uliopita alimaliza na mabao 16, akifuatiwa na Chris Mugalu aliyefunga 15 na mshambuliaji wa Azam FC, Price Dube akimaliza na mabao 14 msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2020/21, hadi sasa hajafunga bao hata moja kwenye ligi hiyo msimu huu huku akionyesha kiwango cha chini.

Akizungumza na gazeti hili, jana Pablo alisema Bocco ni mchezaji mzuri na kinachotokea ni kipindi cha mpito tu na kwamba anaimani anahitaji muda mfupi wa kurejea katika ubora wake.

Alisema hali hiyo inatokea kwa mchezaji kwani kuna wakati inakuwa hivyo, na anachokipitia nyota huyo hakimaanishi hajui bali ni namna ya mchezo anaokutana nao pamoja na ushindani mkubwa.

"Unakuta mchezaji anajipanga na kupania kweli kuhakikisha anafanya kile anachokitarajia katika mechi, na ikitokea akakwama inamuumiza hata yeye mwenyewe.

"Bocco ni mchezaji mzuri na ndio maana ni nahodha, nafahamu namna anavyojisikia kutokana na msimu uliopita alivyofanya vizuri, lakini sasa hajafanya vile," alisema Pablo.

Alisema anaamini kinachotokea kwa mshambuliaji wake huyo ni kipindi cha mpito kwa sababu utafika muda atarejea katika kiwango chake na kufanya vizuri zaidi.

Wakati Pablo akieleza hayo, Bocco amesema suala la kufunga ni bahati na kwamba muda ulifika na Mungu akipanga afunge atafanya hivyo.

"Kikubwa ni kuwa miongoni mwa wachezaji ambao wanacheza Simba, nikipata nafasi ninaipambania timu katika mataji yaliyobaki, mengine muda utazungumza," alisema.

Katika hatua nyingine, Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu, amesema kupoteza mechi dhidi ya Mbeya City, ni kuteleza na kuanguka, lakini hawalali bali wananyanyuka na kusonga mbele kwa kuwa safari bado ni ndefu.

Alisema wamepoteza mchezo wa juzi, lakini hawajapoteza malengo yao kwani yapo pale pale ya kuhakikisha wanatetea ubingwa wao.

"Tumefungwa mechi moja, lakini hatujapoteza malengo yetu yapo pale pale na tunahakikisha tunafanyia kazi kikamilifu zaidi makosa ya leo, (juzi).

"Tunateleza na kuanguka, lakini hatulali tunainuka na kusonga mbele, safari ni ndefu, ligi ina mechi nyingi tunaimani tunaenda kufanya vizuri katika mechi zijazo," alisema Rweyemamu ambaye kitaaluma ni kocha.

Simba ambayo ilipoteza juzi kwa bao 1-0 dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, tayari imerejea jijini Dar es Salaam na wachezaji kupewa mapumziko ya siku moja kabla ya leo jioni kurejea mazoezini kujiandaa na mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar utakaopigwa Januari 22, mwaka huu kwenye dimba na Manungu, Tuliani mkoani Morogoro.

Licha ya kupoteza mchezo huo, bado ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 24, nane nyuma ya Yanga inayoongoza kwenye msimamo wa ligi hiyo, lakini ikiwa mchezo mmoja mbele dhidi ya watani zao hao.

Habari Kubwa