PAC: Lugumi alipewa mkataba kwa 'dezo'

21Apr 2016
Na Waandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
PAC: Lugumi alipewa mkataba kwa 'dezo'
  • Mfumo wa kushindanisha zabuni haukufanyika, Kamati yaamua kuingia yenyewe kazini kujua mbivu na mbichi, ripoti kutinga bungeni kama Escrow ...

BAADA kupitia kwa siku mbili mfululizo taarifa ya serikali ya utekelezaji wa Mkataba wa Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd na Jeshi la Polisi wa ufungaji wa vifaa vya utambuzi wa alama za vidole kwenye vituo vya polisi nchini,..

bunge.

Kamati ya Bunge ya Hesabu ya Serikali (PAC), imebaini madudu mengine kibao ikiwa ni pamoja na zabuni hiyo kutolewa bila ushindani, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo walioshiriki vikao hivyo, walisema wameamua kuunda kamati ndogo ambayo sasa itabidi kupitia hatua kwa hatua mkataba wote pamoja na kutembea nchi nzima kukagua vifaa hivyo kama vimefungwa na vinafanya kazi.

“Juzi tulikutana hatukumaliza, leo tena (jana) na bado hatujamaliza, lakini nadhani kesho (leo), Mwenyekiti wetu (Makamu Mwenyekiti, Aeish Hilary) ataongea na waandishi wa habari awape maazimio. Lakini kiufupi ndiiyo kama nilivyokwambia, tutaunda kamati ndogo ambayo hii sasa lazima ipewe mkataba wote iupitie ili kujiridhisha na mambo ambayo wajumbe wa Kamati hawakuridhika nayo kwenye taarifa ya serikali iliyoletwa,” alisema mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo.

Mjumbe mwingine aliliambia gazeti hili: “Kwanza kupitia taarifa husika, tumegundua kwamba kitengo cha manunuzi cha polisi kilitumia mfumo wa single source (kumpa mtu mmoja kazi bila kuitisha zabuni), halafu hawakuwa na maelezo ya kwanini walichukua hatua hiyo, hawajasema huo mradi ulikuwa na haraka gani mpaka waamue kutumia njia hiyo.

Nyingine alisema ilikuwa ni taarifa iliyowasilishwa haijafafanua kwa kina gharama na utekelezaji wa mradi wenyewe, gharama za uletaji wa vifaa zilikuwaje, kuvifunga vifaa vyenyewe gharama zilikuwaje, mafunzo ya kutumia vifaa hivyo hayajafafanuliwa na kumbuka kuna taarifa kwamba watu watano tu walipewa semina ya kutumia vifaa hivyo kwa Sh. bilioni tano, kwa hiyo lazima kamati ndogo ifanye kazi yake.

Mjumbe mwingine alisema kuwa taarifa hiyo haikuwa na maelezo ya kuridhisha kwamba vifaa hivyo vipo na vinafanya kazi na badala yake iliongeza utata zaidi.

Alisema wakati ripoti ya CAG ikionyesha kuwa vifaa hivyo vilitakiwa kufungwa kwenye vituo vya polisi 108, taarifa iliyowasilishwa bungeni inasema vimefungwa kwenye vituo 194.

“Kamati ndogo itakayoundwa itazunguka kwenye vituo vyote kisha italeta ripoti yake bungeni, hiyo kamati itapewa kila kitu siyo kama walivyosuasua kutuletea hata mkataba, lakini pia wataangalia `value for money' (uhalisia wa mradi na thamani ya fedha zilizotumika),” alisema.

Jana, baada ya kumalizika kwa kikao cha PAC, Aeshi aliwaambia waandishi wa habari kuwa baada ya kufanya mahojiano na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali Projest Rwegasira, leo kamati itaweka kila kitu wazi kwa umma.

Kamati hiyo ilimhoji kiongozi huyo wa serikali aliyesindikizwa na timu ya maofisa wa Jeshi la Polisi kwenye moja ya kumbi za Bunge mjini hapa kuanzia saa 7:00 mchana hadi saa 11:30 jioni.

PAC juzi ililazimika kuwaita bungenini maofisa wa wizara hiyo pamoja na Jeshi la Polisi Tanzania ili watoe ufafanuzi wa mambo mbalimbali kuhusu utekelezaji wa mkataba huo ulioibua gumzo nchini.

Uamuzi wa kuwaita maofisa hao ulifikiwa juzi baada ya kubaini kuna mambo mengi kwenye taarifa ya Wizara ya Mambo ya Ndani iliyotumwa kwenye Ofisi ya Bunge ambayo yalihitaji ufafanuzi wa kina kutoka kwao kuhusu kampuni hiyo.

Kampuni hiyo ilikuwa inatekeleza mradi wa kufunga vifaa vya utambuzi wa alama za vidole kwenye vituo vya polisi nchini.

"Leo (jana) tumemhoji Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. Kamati itamalizia kazi asubuhi, kisha mchana nitawaambia waandishi kuhusu maazimio yetu," alisema Aeshi.

Akizungumza na Nipashe jana jioni, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alisema kamati hiyo ambayo ilipokea taarifa, bado inaendelea na kazi ya kuwahoji wahusika.

Awali, PAC ilisema taarifa ya CAG inaonyesha thamani ya mkataba huo ni Sh. bilioni 37 na ulitakiwa kufunga vifaa hivyo kwenye vituo 108, lakini licha ya kulipwa zaidi ya asilimia 90 ya fedha zote, mpaka sasa wamefunga vifaa hivyo kwenye vituo 14 tu.

Kutokana na hali hiyo, Aprili 5, mwaka huu, kamati hiyo ilitoa siku sita ipewe mkataba wa wabia hao wa kufunga mitambo ya kuchukua alama za vidole nchi nzima.

Habari Kubwa