Panga kali watoa rushwa ubunge CCM

06Aug 2020
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Panga kali watoa rushwa ubunge CCM

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema wanachama wake wote waliojihusisha na rushwa wakati wa mchakato wa kuwania kuteuliwa ubunge na udiwani, watakatwa wakati wa kuteua watakaogombea nafasi hizo.

Vikao vya CCM vinatarajiwa kufanyika wakati wowote kuanzia sasa kuteua wanachama watakaopeperusha bendera ya chama hicho kwenye nafasi za ubunge, uwakilishi kwa upande wa Zanzibar na udiwani katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Katika kura za maoni zilizofanyika hivi karibuni katika maeneo mbalimbali nchini, kuliibuka madai ya baadhi ya wanachama kujihusisha na vitendo vya rushwa. Kutokana na hali hiyo, CCM imesema walioingia katika mkumbo huo watachukuliwa hatua ikiwamo kutopewa nafasi ya kugombea.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi ya CCM, Humphrey Polepole, alisema jana kuwa wanazo taarifa za watu wanachama waliotumia rushwa katika mchakato huo na kwamba watawaadabisha na kuwashangaza.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Polepole alisema katika mchakato wa awali, chama hicho kimeonyesha demokrasia ya hali ya juu hususani kwa kuendesha kwa uwazi mchakato huo japokuwa wapo wachache waliowajaribu.

“Nafahamu kwenye uchaguzi huwa kuna mambo mengi, lakini jambo moja nalijua, kwamba uchaguzi wa CCM unaongozwa na Katiba na Kanuni. Yale ambayo tumekatazwa, yasifanywe.

“Unyenyekevu wa viongozi wakati wote wa uchaguzi si jambo la mjadala. Ningependa ifahamike na napenda kuwahakikishia wana- CCM wote tuko vizuri sana na wale wachache ambao wamejaribu…jaribu.. kutujaribu, tutawashangaza. Nasema tutawashangaza,” alisema.

“Chama hiki mwaka 2016 katika Mkutano wake Mkuu Maalum uliofanyika Agosti, halafu Halmashauri Kuu iliyofanyika Desemba 12 na 13, kilifanya uamuzi wa kihistoria kwa kufanya mageuzi makubwa ya kiuongozi, kioganizesheni na kiutendaji. Kazi kubwa ambayo imefanyika imekirejesha chama kwenye ramani ya siasa na uongozi wa Tanzania,” aliongeza Polepole.

Alisema chama hicho kitaendelea kusisitiza na kusimamia msimamo wake huo kwa kuhakikisha Katiba, Kanuni na taratibu za chama zinafuatwa na kuzingatiwa na kwamba viongozi wanaowataka ni wale tu ambao ni waadilifu.

“Ndiyo maana kwa kazi hii ya mageuzi makubwa katika maeneo hayo matatu, tunataka viongozi waaminifu, waadilifu, wachapakazi, wanaochukizwa na rushwa, na kwetu sisi rushwa ni jambo linalokataliwa kimsingi. Sasa ni vizuri wakati mwingine viongozi pia wakafundishwa adabu. Tutafundisha watu adabu kipindi hiki,” alisisitiza.

Alisema katika kupata wagombea, wataweka rekodi kwamba walipata kuwapo viongozi kwenye chama ambao waliwakumbusha vikali watu ambao wanashindwa kuelewa utaratibu na waliokiuka walichukuliwa hatua.

Polepole alisema watu ambao walidhani kwamba chama hicho kutangaza kupiga vita rushwa katika mchakato wa uchaguzi ilikuwa si halisi, basi katika kipindi hiki watashangazwa.

“Katika kituo chetu kile cha taarifa za uchaguzi, tunapokea taarifa nyingi. Nasema kipindi hiki tutawashangaza watu waliodhani kwamba ni ‘business as usual’ (mambo ya yanakwenda kwa mazoea) inaendelea kwenye chama hiki. Wana-CCM wawe na amani, ushindi mkubwa unakuja.

“Wanachama walioomba dhamana ya uongozi ambao wamefuata na kuzingatia Katiba na Kanuni na hawakujihusisha katika makatazo na miiko, wawe na amani na watulivu. Mwenyekiti na safu yote ya uongozi, wanatambua unyenyekevu wao na sisi hatutawaangusha watu waaminifu na wenye nidhamu,” alisema Polepole.

Aliongeza kuwa: “Ila wale mliopiga mazonge tutafundisha watu adabu kipindi hiki. Sipendi kusema maneno mengi kwa sababu pia unapofundishwa adabu ni vizuri ukaipata ‘by surprise’ (kwa kushtukiza). Unasema ee imekuwa hivyo, ndiyo imekuwa hivyo mjomba, imeisha hiyo, utafute kazi nyingine. Uongozi unaotweza misingi ya Katiba ya chama chetu hauna nafasi. Kwa hiyo wana-CCM, tulieni.”

JPM KUCHUKUA FOMU

Polepole alisema Mwenyekiti wa Chama hicho, Rais John Magufuli anatarajia kuchukua fomu ya kugombea urais wiki hii.

“Rais Magufuli atachukua fomu wiki hii na siku atakayochukua nitawatangazia ili wote macho yetu yawe pale wakati ndugu yetu kwa mara ya pili akiomba dhamana baada ya kuwa amefanya kazi nzuri sana iliyotukuka na iliyovunja rekodi si tu Tanzania bali duniani,” alisema.

Pia alisema wameridhika na maandalizi ya uchaguzi kwa upande wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Habari Kubwa