Panga lafyeka vigogo wa CCM

15Jan 2023
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Panga lafyeka vigogo wa CCM

PANGA limefyeka vigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kauli hiyo inasadifu mabadiliko makubwa ambayo Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama hicho imeyafanya katika sekretarieti.

Rais Dk. Samia Samia Suluhu Hassan.

Mabadiliko hayo yalitangazwa jana baada ya  kumalizika kwa kikao cha NEC kilichofanyika jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wa Taifa, Rais Dk. Samia Samia Suluhu Hassan. Katika mabadiliko hayo, wajumbe wawili tu wa Sekratarieti ya NEC ndio waliorejea katika nafasi zao huku wengine wakiondolewa.

Akitangaza mabadiliko hayo, aliyekuwa Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, alisema Katibu Mkuu, Daniel Chongolo na Katibu wa NEC, Uchumi na Fedha, Dk. Frank Hawassi, wanaendelea kubaki katika nafasi hizo.  

Wakati Chingolo na Dk. Hawassi wakibaki, Naibu Makatibu Wakuu, Christine Mndeme (Bara) na Abdallah Juma Sadalla ‘Mabodi’ (Zanzibar), wameondolewa kwenye nyadhifa hizo.

Wakuu wa idara, mbali na Shaka, wengine walioondolewa ni Dk. Moudline Castico (Oganaizesheni), Kanali Hezron Lubinga (Siasa na Uhusiano wa Kimataifa).

Hata hivyo, Mndeme, Shaka na Mabodi wanaendelea kuwa wajumbe wa NEC kutokana na ushindi walioupata katika uchaguzi uliofanyika wakati wa Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM uliofanyika mwezi uliopita jijini Dodoma. Castico na Lubinga walibwagwa katika kinyang’anyiro cha ujumbe wa NEC.  

Walioteuliwa kujaza nafasi za waliotemwa katika sekraterieti ni Anamringi Macha ambaye anakuwa Naibu Katibu Mkuu (Bara) na Mohamed Said Mohamed, maarufu kama Dimwa anayechukua nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Zanzibar.

Makatibu na wakuu wa idara wapya walioteuliwa na nyadhifa zao kwenye mabano ni Sophia Mjema (Itikadi na Uenezi), Mbarouk Nassor Mbarouk (Siasa na Uhusiano wa Kimataifa)  na Issa Haji Ussi, maarufu kama Gavu (Oganaizesheni).

Kabla ya uteuzi huo, Mjema alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga wakati Anamringi Macha ni ofisa mkongwe ndani ya CCM na aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kahama. Katika uchaguzi wa kinyang’anyiro cha NEC, Macha aliibuka kidedea katika kundi la Tanzania Bara.

KAMATI KUU MPYA

Mbali na kufanya mabadiliko katika sekretarieti, NEC pia imeteua wajumbe sita kuunda Kamati Kuu (CC-NEC), watatu kutoka Zanzibar na wengine kutoka Tanzania Bara.

Walioteuliwa kwa Zanzibar ni Mohamed Aboud Mohamed, Mhandisi Nassir Ali Juma na Laila Burhan Ngozi. Aboud alishawahi kuwa Naibu Waziri wa Mambo na Ndani ya Nchi na baadaye iliyokuwa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika serikali ya awamu ya nne ya Tanzania kabla ya kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar.

Kwa upande wa Tanzania Bara, walioteuliwa ni Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda ambaye alikuwamo katika Kamati Kuu iliyomaliza muda wake, Hassan Wakasuvi na Halima Mamuya.

Mamuya aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ambao ni moja ya Jumuiya za CCM pamoja na Mbunge wa Viti Maalum wa chama hicho.

YAJAYO MAKUBWA

Baada ya mabadiliko hayo ndani ya Chama, macho na masikio ya Watanzania ni kwa Rais Dk. Samia katika kuendelea kutekeleza ahadi yake ya kuisuka serikali kwa kufanya uteuzi kwenye nafasi mbalimbali.

Rais Samia aliomba rai kwenye Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM kuwa anaomba kuisuka serikali ili kuteua watu watakaoendana na kasi yake ya kutaka kuwaletea Watanzania maendeleo.

Alianza kufanya hayo hivi karibuni baada ya kufanya mabadiliko makubwa ndani ya Ikulu baada ya kumteua Dk. Moses Kusilika kuwa Katibu Mkuu Kiongozi. Kabla ya uteuzi huo, Dk. Kusiluka alikuwa Katibu Mkuu, Ikulu.

Dk. Kusiluka alichukua nafasi ya Balozi Hussein Katanga aliyeteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania, New York nchini  Marekani na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Ofisi za Umoja wa Mataifa, New York.

Rais Samia alimteua aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Kamishna Diwani Athumani kuwa Katibu Mkuu, Ikulu huku nafasi yake ikichukuliwa na Said Hussein Masoro ambaye kabla alikuwa Naibu Mkurugenzi Mkuu na Mkurugenzi wa Shughuli za ndani wa idara hiyo.

Hata hivyo, uteuzi wa Diwani ulitenguliwa saa 43 baada ya kuteuliwa kwake na nafasi yake ikachukuliwa na Mulili Mahendeka, aliyekuwa ofisa mwandamizi Ikulu.

Habari Kubwa