Pangua pangua yatikisa Magereza

08Jan 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Pangua pangua yatikisa Magereza

MTIKISIKO mkubwa wa mabadiliko umeibuka ndani ya Jeshi la Magereza, baada ya Kaimu Kamishna Jenerali wa Jeshi hilo, Dk. Juma Malewa, kuwapangua maofisa waandamizi wakuu wa chombo hicho katika mikoa na makao makuu.

Taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Habari wa Magereza, Mrakibu Msaidizi wa Magereza (ASP) Lucas Mboje, inaonyesha kuwa katika mabadiliko hayo, baadhi ya vigogo wameondolewa kwenye nafasi zao na baadhi kupandishwa.

Katika mabadiliko hayo, aliyekuwa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Morogoro Kamishna Msaidizi Mwandamizi (SACP) Katos Rugainunura, amehamishiwa Makao Makuu ya Magereza sehemu ya utawala na nafasi yake inakaimiwa na Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP), Mzee Nyamka aliyekuwa Mkuu wa Utawala Magereza Mkoani Morogoro.

Mabadiliko hayo yamemgusa SACP Antonino Kilumbi aliyekuwa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Dodoma ambaye amehamishwa Makao Makuu ya Magereza kuwa Mkuu wa Kikosi cha Ujenzi. Nafasi yake inachukuliwa na SACP Julius Sang’udi aliyekuwa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mbeya.

Aliyekuwa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Kilimanjaro, ACP Anderson Kamtiaro, amepelekwa kuwa Ofisa Mnadhimu Mkoa wa Arusha na nafasi yake inachukuliwa na ACP Hassan Mkwiche ambaye alikuwa Mkuu wa Gereza Kuu Karanga, Moshi.

Aliyekuwa Mkuu wa Gereza la Same, ACP Evarist Katego anahamishiwa kuwa Mkuu wa Gereza Kuu Karanga, wakati aliyekuwa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mwanza, SACP Uwesu Ngarama, amehamishiwa Makao Makuu kuwa Boharia Mkuu na nafasi inachukuliwa na aliyekuwa Ofisa Mipango wa Jeshi, ACP Athuman Kitiku.

Taarifa hiyo ilibainisha kuwa aliyekuwa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mtwara, ACP Musa Kaswaka anakwenda Makao Makuu Kitengo cha Ukaguzi na nafasi yake kuchukuliwa na ACP Ismail Mlawa aliyekuwa Mkuu wa Kiwanda cha Samani Gereza Kuu Ukonga na aliyekuwa Ofisa Mdhibiti wa Fedha wa Jeshi, SACP Gideon Nkana anakwenda kuwa Mkuu wa Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji, Ukonga, Dar es Salaam na nafasi yake kuchukuliwa na ACP Chacha Jackson.

Wengine ni pamoja na aliyekuwa Ofisa Mnadhimu wa Magereza Mkoa wa Mbeya, ACP Kijida Mwakingi, anakuwa Kaimu Mkuu wa Magereza Mkoa huo wakati ACP Abdallah Misanga anayetoka Gereza la Mgumu anahamishiwa Gereza la Msalato kuendelea na wadhifa huo na ACP John Itambu anatoka Gereza la Kilosa kwenda kuwa Mkuu wa Kiwanda cha Samani Gereza Kuu Ukonga.

“ACP Erasmus Kundy anayetoka Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Ukonga kwenda Makao Makuu Kitengo cha Habari, ACP Julius Ntambala aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Ujenzi Makao Makuu anabakia Makao Makuu Kitengo cha ujenzi kuwa Msaidizi wa Mkuu wa Kitengo. ACP Sylivester Mrema anatoka Gereza la Idete kwenda Gereza la Ubena kuwa Mkuu wa Gereza,” ilisema taarifa hiyo.

Aidha, Mkuu wa Gereza la Ubena, ACP Shaba Zephania, anakwenda Magereza Mkoa wa Pwani kuwa Ofisa Mnadhimu, ACP Solomon Urio anatoka Makao Makuu kwenda Magereza Mkoa wa Dar es Salaam kuwa Ofisa Mnadhimu na Boharia Mkuu wa Jeshi, SACP George Kiria, amehamishiwa Makao Makuu Kitengo cha Uhasibu.

Pamoja na kwamba mabadiliko hayo yamesababisha mtikisiko kutokana na kufanyika siku chache baada ya kustaafu kwa aliyekuwa mkuu wa jeshi hilo, Kamishna Jenerali John Minja, Mboje alisema katika taarifa hiyo kuwa ni ya kawaida na yanalenga kuboresha utendaji kazi na ufanisi.

Habari Kubwa