PASS kuwezesha mikopo 1,260,000 wajasiriamali

01Aug 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
PASS kuwezesha mikopo 1,260,000 wajasiriamali

UONGOZI wa Asasi ya PASS, umesema unajivunia kusaidia ukuaji wa sekta ya kilimobiashara nchini tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000, ikiwezesha upatikanaji wa mikopo ya mabilioni ya shilingi kwa wajasiriamali katika sekta hiyo.

Vilevile, asasi hiyo iliyoanza kazi zake rasmi nchini mwaka 2007 kwa lengo la kuwezesha maendeleo ya wajasiriamali katika sekta ya kilimobiashara, imepanga kuwezesha mikopo 1,267,800 kwa wajasiriamali katika sekta hiyo kufikia mwaka 2022.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa PASS, Nicomed Bohay, asasi hiyo katika kutekeleza majukumu yake, imekuwa ikishirikiana benki 13 zikiwamo CRDB, Akiba, BoA, Amana, NBC, Equity, Mkombozi, Access, Azania, TPB, na TADB.

Bohay alibainisha jana kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka huu (Januari hadi Machi 2020), mikopo yenye thamani ya Sh. bilioni 71.5 ilikuwa imetolewa kwa wajasiriamali kwa udhamini wa PASS.

Alisema kuwa, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2000 hadi Machi 31 mwaka huu, jumla ya miradi 36,007 yenye thamani ya Sh. bilioni 916.4 ilikuwa imeidhinishiwa mikopo kwa udhamini wa PASS, ikihusisha wajasiriamali 1,196,891 walionufaika.

"Inafurahisha zaidi kwamba kati yao, asilimia 45 ni wanawake. Wajasirimali hawa ni wakulima, Vyama vya Kuweka Akiba na Kukopa (SACCOS), mashirika na vyama vya wakulima, kampuni na mjasiriamali mmoja mmoja anayejihusisha na kilimobiashara," alisema.

Bohay alibainisha kuwa, licha ya mlipuko wa corona uliokuwa tishio zaidi Januari na Machi mwaka huu, PASS imewezesha kuanzishwa kwa miradi 4,404 yenye mikopo kwa wanufaika 41,030 (asilimia 65 wakiwa ni wanaume).

Takwimu za Benki Kuu (BoT) mwaka huu zinaonyesha PASS imetoa mchango mkubwa katika sekta ya kilimo nchini. Kwa mujibu wa BoT, kati ya mikopo 8,285,831 iliyotolewa na benki kwa sekta ya kilimo nchini kati ya mwaka 2013 na Novemba 2019, mikopo 956,298 ilidhaminiwa na PASS.

Bohay alisema kuwa, katika kuunga mkono jitihada za serikali katika kukuza uchumi wa nchi, PASS katika mikakati yake ya mwaka 2018-2022, imepanga inawezesha mikopo walau 1,267,800 kwa wajasiriamali katika sekta ya kilimobiashara na kupunguza tatizo la ajira nchini.

"Pia tumepanga kuongeza kiwango cha mikopo tunayoidhamini kutoka Sh. bilioni 126 kwa mwaka (2018) hadi kufikia Sh. bilioni 184 mwaka 2022 na kutoa mikopo zaidi kwa wajasiriamali wanawake," alisema.

Alisema malengo mahususi kwa mwaka huu (2020) ni kuyafikia makundi muhimu hasa kuwawezesha vijana na wanawake kujikwamua kiuchumi kupitia kilimobiashara.

Habari Kubwa