PASS Trust na Benki ya Equity waingia makubaliano udhamini wa mikopo

13Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
PASS Trust na Benki ya Equity waingia makubaliano udhamini wa mikopo

Taasisi ya PASS Trust na Benki ya Equity wametia saini mkataba wa jumla ya Tsh. bilioni 2.3 kwaajili ya ushirikiano wa udhamini wa mikopo ya kilimo yenye lengo la kuwasidia wakulima wa chini ambao wamekosa dhamana kutokana na kukosa vigezo na kushindwa kufikia kilimo cha kibiashara.

Mkurugenzi wa PASS TRUST, Yohane Kaduma na Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Equity, Robert Kiboti wakibadilishana mkataba wa makubaliano ya ushirikiano wa udhamini wa mkopo ya kilimo.

Taasisi ya PASS Trust na Benki ya Equity kwa kushirikiana wametia saini mkataba wa jumla ya Tsh. bilioni 2.3 kwaajili ya ushirikiano wa udhamini wa mikopo ya kilimo yenye lengo la kuwasidia wakulima wa chini ambao wamekosa dhamana kutokana na kukosa vigezo na kushindwa kufikia kilimo cha kibiashara.

Akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba huo iliyofanyika leo, Mkurugenzi Mtendaji wa PASS Trust, Yohane Kaduma, amesema makubaliano hayo ni muhimu kwa wafanyabiashara wa kilimo nchini, na pia ni habari njema kwa wanaojihusisha na kilimo, uvuvi, na ufugaji na shughuli zote katika minyororo ya thamani katika sekta hizo.

"Katika kuanzisha uhusiano huu na benki ya Equity, PASS, tumetoa takriban dola million moja za kimarekani ( I,000,000 USD) kwa benki hii ya equity, kwa ajili ya kudhamini mikopo ambayo itatolewa na benki hii kwa wakulima mbalimbali wanaojihusisha na kilimo biashara kote nchini.," amesema Kaduma na kuongeza kuwa;

"Udhamini huu ni sawa na pesa zetu za Kitanzania ambazo ni takriban shillingi billioni 2.3 na ina uwezo wa kudhamini mikopo ya mpaka billioni 13.

Ushirikiano huu ni moja wapo ya hatua za PASS kuwafikia wakulima kwa lengo la kuwainua kutoka wimbi la umaskini.Naishukuru benki ya Equity, ikiongozwa na Mkurugenzi wake Bw. Robert Kiboti, kwa kutuamini na kukubali kufanya kazi nasi, ili kuwawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi nchini.," amesema Kaduma 

Amesema kuwa ili kutimiza lengo hilo, PASS inafanya kazi na benki 14 nchini, na benki ya Equity ikiwa ndiyo benki mpya zaidi kuingia katika makubaliano na taasisi hiyo siku ya leo, kwa ajili ya kuendeleza udhamini wa mikopo  ya kilimo biashara.

"Watu tunaowahudumia ni pamoja na wajasiriamali binafsi wa biashara za kilimo, vyama / makundi ya wakulima wadogo wadogo na makampuni yanayojihusisha na sekta ya kilimo. Pamoja na mambo mengine, tunawasaidia wateja wetu katika kuandaa miradi bora ya uwekezaji ambayo inaweza kuwapatia faida kubwa na kuwezesha upatikanaji wa huduma za fedha kwa ajili ya kuifadhili miradi hiyo kupitia udhamini wa mikopo kwa kushirikiana na benki za kibiashara.," amesema 

Ameongeza kuwa tangu kuanzishwa mwaka 2000, Jumla ya wajasiriamali million 1.7 wamefaidika na mikopo iliyodhaminiwa na PASS kupitia mikopo yenye thamani ya shillingi trillioni 1.219, pia ajira takriban million mbili na laki sita  zimetengenezwa kutokana na miradi hii ambayo imedhaminiwa na PASS Trust.

"Ni muhimu kutambua kwamba katika mwaka wa 2020 pekee, PASS ilinufaisha jumla ya biashara 532,798 zinazojihusisha na mazao na huduma kwenye kilimo kupitia udhamini wa mikopo na huduma za maendeleo ya biashara katika mikoa  yote nchini. Mikopo hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha na kupanua wigo wa biashara za mazao na huduma katika kilimo nchini.," amesema 

Hata hivyo Kaduma ametoa wito kwa wakopaji watakaonufaika na mikopo yenye udhamini wa PASS kwenye benki ya Equity kuwa waadilifu katika ulipaji ili benki zote washiriki ziweze kuendelea kutoa mikopo kwa watanaznia wengi zaidi.

PASS trust ni taasisi iliyoanzishwa mwaka 2000 na serikali ya Jamhuri ya m,uungano wa Tanzania na Denmark ambayo inayojihusisha kudhamini wakulima pamoja na vikundi au taasisi zinazojihusha na kilimo.