PIDO yawafunza wasichana mila kandamizi, ndoa za utotoni

16Aug 2019
Zanura Mollel
LONGIDO
Nipashe
PIDO yawafunza wasichana mila kandamizi, ndoa za utotoni

SHIRIKA la Maendeleo ya Jamii (PIDO) limetoa mafunzo kwa wasichana zaidi ya 70 wenye umri kuanzia miaka 11 hadi 17 juu ya athari za ndoa na mimba za utotoni.

Mkurugenzi Wa shirika la PIDO Bi Martha Ntoipo akizunguza na Wasichana hao katika ukumbu Wa Tembo Trust Wilayani Longido.

Mkurugenzi wa Shirika hilo, Martha Ntoipo amesema PIDO lilianza kufanya shughuli zake tangu mwaka 2010 na wamejikita katika masuala ya elimu juu ya afya ya uzazi,vita dhidi ya mimba na ndoa za utotoni, madhara ya ukeketaji pamoja na mafunzo juu ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (HIV).

Martha amesema kuwa kutokana na Serikali kuweka zuio kwa wanafunzi wanaopata mimba kuendelea na masomo shirika hilo limeona ni vyema kuzungumza na wasichana hao ili waweze kujilinda na kuhakikisha wanafikia malengo yao ya kielimu.

"Tumeona tutibu tatizo kabla halijakua kubwa, watoto hawa wafahamu madhara ya mimba na ndoa za utotoni, tunaamini watapokea na mabadiliko yataonekana," amesema Martha

Wasichana waliohudhuria katika mafunzo hayo.

Ameongeza kuwa baadhi ya mila na desturi kandamizi kwa jamii ya kifugaji (maasai) imekua ikikwamisha malengo mbalimbali ya serikali ikiwemo upande wa afya ambapo serikali imezindua kampeni ya kuwavusha wanawake salama., ila inaweza kutoleta mafanikio kutokana na mila hizo.

"Kuwavusha wanawake salama, akina mama wajawazito ni malengo ya serikali, ila mila zinakwamisha, mfano mimba za utotoni, ndoa za utotoni pamoja na ukeketaji, wanawake wengi wanapoteza maisha, vifo vya mama na mtoto kutokana na kushindwa kumudu afya ya uzazi, yote hiyo ni mila na desturi kandamizi," -amesema

Ikumbukwe kuwa June 21, mwaka huu Mkuu wa Wilaya ya Longido Mkoani Arusha, Frank Mwaisumbe alizindua kampeni ya JIONGEZE TUWAVUSHE SALAMA iliyobeba dhamira ya kuokoa maisha ya mama na mtoto kabla na baada ya kujifungua, na kuwataka wakina mama wajawazito kuacha tabia ya kujifungulia majumbani.

Mwaisumbe alieleza kuwa ili tuweze kufikia malengo ya kitaifa  80% ya kupunguza vifo vya mama na mtoto kuna umuhimu wa kutoa Elimu kwa jamii pamoja na kuhakikisha vifaa tiba vinapatikana katika vituo vyetu  vya afya.

" Tuhakikishe tunao wakunga wakutosha kwenye vituo,wahudumu Wa afya pamoja na madaktari vikiambatana na vitendea kazi," alisema Mwaisumbe.

Mratibu  Kitengo cha afya ya uzazi mama na mtoto wilayani hapa,  Josiah Mruve alipokua akiwasilisha taarifa kwa Mkuu wa Wilaya, Mwaisumbe, alisema kiwango cha wakina mama  kujifungulia katika vituo vya afya kimeongezeka kutoka asilimia 27 mwaka 2017 hadi asilimia 51.3 mwaka 2019, 

"Lakini pia kumekuwa na ongezeka la wanaume kuhudhuria kliniki na wake zao kwa asilimia 59.2 tofauti na miaka ya nyuma hii ni dhairi wamekua na uelewa juu ya afya ya uzazi" alisema

Hata hivyo alifafanua kuwa wakinamama waliohudhuria kliniki wakiwa na mimba chini ya wiki 12 mwezi octoba_desemba 2018 ilikua asilimia 38 lakini kwa sasa imepanda hadi 43.6 asilimia,na hii ikiwa ni miongoni mwa viashiria vya ngazi ya kitaifa juu ya afya ya uzazi.

Kwa upande wa utoaji wa dawa za SP kwa ajili ya tiba kinga ya malaria kwa mama mjamzimto kwa mwezi January_march mwaka 2019 ni kwa 99.4 asilimia huku utoaji Wa vyandarua ikiwa ni kwa asilimia 100 kwa wajawazito wote waliohudhuria kliniki.

Aidha alieleza kuwa kumekuwa na changomoto ya lishe kwa watoto huku utapia mlo ukionekana kushika kasi wilayani hapa na kuwataka viongozi kwa kushirikiana na wadau mbali mbali kuhakikisha taswira hii inapotea kwani malengo ya kitaifa hayaruhusu kufikia asilimia 2. 

" Watoto Elfu 7431 walipimwa afya na kupata chanjo ,watoto Elfu 6438 walikua na lishe nzuri sawa na asilimia 86 , rangi ya kijivu walikua watoto 841 sawa na asilimia 11 huku kwenye lishe duni wakiwa ni watoto 152 sawa na asilimia 2, -alisema Mruve

Mruve alisema wakina mama wajawazito waliohudhuria kliniki walipimwa maambukizi ya VVU (UKIMWI) kwa asilimia 99.5 na kiwango cha waliobainika kuambukizwa ilikua asilimia 0.4 ,na wote walianzishiwa dawa za kufubaza Virusi hivyo.