Pigo mali za Mbowe kunadiwa

05Jul 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Pigo mali za Mbowe kunadiwa

NI pigo lingine. Ndivyo inavyoweza kuelezwa juu ya Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, kutokana na taarifa kuwa mali zake zinatarajiwa kupigwa mnada.

Freeman Mbowe.

Mali za kigogo huyo na Mbunge wa Hai, zimetangazwa kuuzwa kwa njia ya mnada kesho ili kulipa deni la miaka mitatu iliyopita la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa jana na Dalali wa Mahakama, Kampuni ya Udalali ya Fosters Auctioneers and General Traders ya Dar es Salaam, Joshua Mwaituka, watauza kwa mnada vitu vyote vilivyokuwa mali za Mbowe Limited (Bilicanas).

Mnada huo unahusisha mali zilizokuwa kwenye ukumbi wa Bilicanas ambako mwaka 2016, NHC ilizichukua kwa maelezo kuwa kampuni hiyo ya Mbowe haijalipa kodi kwa miaka 20.

Tangazo la kampuni ya udalali, lilieleza kuwa mnada huo utafanyika asubuhi kwenye ghala la NHC lililoko jirani na ofisi za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) karibu na gati namba 3 la Bandari ya Dar es Salaam.

Akizungumza na Nipashe, Mwaituka alisema kazi waliyopewa ni kuuza mali ambazo ni makochi, meza, kabati, friji na vitu vya alminium.

Alipoulizwa kuhusu deni ambalo inadaiwa kampuni hiyo ya Mbowe ni kiasi gani hadi sasa, Mwaituka alisema wanaohusika kujibu ni NHC wenyewe.

“Kazi yangu ni kuuza vitu vyote vilivyokuwa mali ya Mbowe Limited (Bilicanas). Kama amelipa au hajalipa waulizwe NHC. Sisi kazi yetu ni kupiga mnada ambao utafanyika Jumamosi (kesho),” alisema.

Gazeti hili lilipomtafuta Japhet Mwanasenga kutoka NHC, kwa lengo la kujua deni linalodaiwa hadi sasa ni kiasi gani, alisema anayeweza kujibu ni Meneja Mawasiliano wa NHC, Yahya Cherehani, ambaye naye alitafutwa bila mafanikio.

Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi, wakati wote ilikuwa imezimwa ndipo Mkuu wa Idara ya Habari wa Chadema, Tumaini Makene, aliliambia gazeti hili kuwa yuko mahakamani.

Mwaka 2016, NHC iliondoa vifaa vyote vilivyokuwa vinavyotumiwa na Kampuni ya Free Media na kufungua vifaa vyote vya muziki kwenye klabu ya Bilicanas kwa maelezo kuwa anadaiwa pango zaidi ya Sh. bilioni 1.7.

Habari Kubwa