Pinda afunga maadhimisho ya siku ya nyuki

21May 2022
Neema Hussein
Nipashe
Pinda afunga maadhimisho ya siku ya nyuki

Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda  amewataka wananchi kutumia fursa zilizopo katika sekta ya nyuki  ili kuinua  pato la nchi na mtu mmoja mmoja kupitia  biashara  mbalimbali zitokanazo na mazao ya nyuki.

Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda akizindua muongozo wa namna ya kutumia makundi ya nyuki kwenye uchavushaji wa mazao ya nyuki.

Pinda ameyasema hayo katika kilele cha maadhimisho ya siku ya nyuki duniani ambayo kitaifa yamefanyika mkoani Katavi  huku akileza umuhimu wa kutunza mazingira kwa maslahi mapana ya nchi na kufanya nyuki wazalishe asali kwa wingi.

Hatahivyo Pinda ameomba wadau mbalimbali kama vile SIDO na TBS kusaidia kutoa elimu kwa vikundi mbalimbali ili kuwawezesha kupiga hatua katika masoko ya kimataifa  na kuongeza uelewa wao katika maswala ya nyuki.

"Niwatake tu wakuu wa mikoa mliohudhulia hapa na wengine pia kutopuuza uharibifu wa mazingira kwasababu nyuki zinauhusiano mkubwa sana na mazingira na zinaishi kwa kutegemea mazingira,"alisema Mizengo Pinda.

Pinda pia amezindua muongoza wa namna ya kutumia makundi ya nyuki kwenye  uchavushaji wa mazao ya nyuki na kaulimbiu ya mwaka huu inasema "nyuki ni uchumi tuwalinde na tuhifadhi mazingira yao".

Nae Mkuu wa mkoa wa Katavi  Mwanamvua Mrindoko amesema changamoto za ufugaji nyuki nipamoja na muamko mdogo wa wananchi,  upungufu wa watumishi katika sekta hiyo, uharibifu wa Mazingira yaliyotengwa kwaajili ya  ufugaji wa nyuki.

Amesema mikakati ya mkoa huo ni kuongeza uzalishaji wa nyuki,kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu uzalishaji wa mazao ya nyuki, kuhakikisha  wachakataji wanapata vifungashio,na kuongeza viwanda vya kuchakata mazao ya nyuki katika mkoa

"Sekta hii ya ufugaji nyuki nimoja kati ya sekta muhimu ya uzalishaji wa kiuchumi katika mkoa wetu wa Katavi  ambapo kwa kipindi cha miaka mitano sekta hiyo imeingizia sh. 13.4 bilion  kwamaana ya asali Camila na mazao mengine ya nyuki,"alisema Mrindoko.

Kwaupande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Ufugaji Nyuki Tanzania Jackson Msome, amesema halmashauri nyingi hazina maafisa nyuki isipokua wengi ni makaimu hivyo amewataka wakurugenzi wa halmashauri  kuajili maafisa nyuki ili sekta  hiyo iweze kusonga mbele.

Frolence Samizi Mbunge wa Jimbo la Muhambwe mkoani Kigoma ameishauri Wizara ya Maliasili na Utalii kutoa semina maalumu kwa wakurugenzi wa halmashauri ili wajue umuhimu wa ufugaji nyuki kwenye halmashauri zao.

Habari Kubwa