Pinda akumbusha ubora elimu

23Mar 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Pinda akumbusha ubora elimu

Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Mizengo Pinda, amesisitiza umuhimu wa elimu katika kufanikisha malengo ya nchi ikiwamo kufikia uchumi wa kati na viwanda.

Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Mizengo Pinda.

Pinda aliyasema hayo wakati wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na Chuo Kikuu Huria cha China, yaliyofanyika makao makuu ya muda ya hicho, Dar es Salaam.

Alisema ili kufikia uchumi wa viwanda Tanzania haina budi kuhakikisha ina rasilimali watu ya kutosha na yenye sifa katika kukabiliana na mapinduzi ya uchumi wa viwanda.

“Lengo la nchi kufikia uchumi wa kati na viwanda litafanikiwa endapo wananchi wote watapata elimu ili kuendana na kasi ya ukuaji wa uchumi,” alisema.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Profesa Elifas Bisanda, alisema makubaliano hayo yanalenga kuwaweka Watanzania karibu na Wachina ili kubadilishana uzoefu na kujifunza mambo mbalimbali ya kitaaluma na kiutamaduni.

“Tutashirikiana na watu wa China katika masuala ya utamaduni kama vile kujifunza lugha na teknolojia ili kujijengea uwezo wa kufundisha kwa kutumia Tehama,” alisema Bisanda.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais Chuo Kikuu Huria cha China, Profesa Yang Xiaotang, alisema urafiki kati ya Tanzania na China ni wa muda mrefu na kuwa ni chuo cha kwanza kushirikiana na chuo hicho.

“Tutashirikiana kujenga majengo yatakayosaidia wanachuo kupata mafunzo kupitia Tehama kwa teknolojia rahisi zaidi,” alisema Profesa Yang.

Profesa Yang alisema ujenzi wa majengo hayo utafadhiliwa na Chuo Kikuu Huria cha China kupitia Ubalozi wa China Tanzania na Benki ya Exim.

Habari Kubwa