Pinda ataka shule yake iwe kituo afya

03Jan 2018
Gurian Adolf
Nipashe
Pinda ataka shule yake iwe kituo afya

WAZIRI Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, amependekeza Shule ya Msingi Kakuni iliyopo Kijiji cha Kibaoni aliyokuwa ameijenga kupitia misaada ya wafadhili akiwa madarakani kuwa kituo cha afya.

WAZIRI Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda.

Mapendekezo hayo aliyatoa katika sherehe za kuuaga mwaka 2017 na kuukaribisha mwaka mpya 2018 zilizofanyika Mjini Mpanda na kuandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari mkoani Katavi kwa kushirikiana na baadhi ya wadau.

Lengo kubwa la kubadilisha matumizi ya shule hiyo mpya ambayo haijawahi kutumika na imejengwa kisasa, ni kuchangia jitihada za serikali katika kuboresha huduma ya afya mkoani Katavi na Tanzania kwa ujumla na kupongeza jitihadi ambazo serikali inaendelea kuzifanya katika kuboresha huduma za afya.

Majengo hayo yana jumla ya vyumba vya madarasa 26, nyumba za kuishi walimu 24, nyumba ya utawala, maktaba 2, eneo zuri la chumba cha kompyuta na kituo cha walimu kujifunzia, hivyo kama pendekezo hilo litapitishwa na serikali, kituo hicho kitapokea wauguzi kutoka mikoa mbalimbali.

Pinda pia alipongeza huduma za afya zinazotolewa na serikali katika Kituo cha Afya cha Mamba katika Wilaya ya Mlele mkoani Katavi ambapo zaidi ya watu 73,000 wanapatiwa huduma kwa mwezi huku, kinamama zaidi ya 180 wakijifungua kwa njia salama na 10 hadi 15 wakifanyiwa upasuaji licha ya kituo hicho kuwa na idadi ndogo ya watumishi.

Alisema huduma za uzazi wa mama na mtoto haziridhishi na kuwataka viongozi wa serikali kuendelea kutoa msukumo katika suala hilo kwani bado nguvu inahitajika hasa katika mikoa mipya ambayo imekuwa ikipata ongezeko la watu kwa kasi kubwa na kutoa mfano wa Mkoa wa Katavi, ambao alisema kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, ulikuwa na zaidi ya watu 500,012 wakati kwa sasa unakisiwa kuwa na watu kati ya 600,000 na 700,000.

Aidha, Pinda alipongeza jitihada za serikali kupitisha mradi wa ujenzi wa barabara ya lami kutoka mkoani Tabora kwenda Mpanda ambao unatarajiwa kuanza hivi karibuni na kampuni tatu za Kichina zimeingia mkataba na serikali.

Alishauri mradi huo utapoanza uwashirikishe wananchi wa maeneo hayo, ili kunufaika pamoja na mradi wa reli kuanzia Kaliua kwenda Karema.

Naye mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Katavi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Lilian Matinga, alipongeza hatua ya Pinda kupendekeza shule hiyo kuwa chuo cha wauguzi, akisema ni wazo zuri na kupongeza jitihada zinazoendelea kufanywa na serikali za kuletea wananchi maendeleo.