Pingamizi lawakumba 'Samaki wa Magufuli'

24Nov 2016
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Pingamizi lawakumba 'Samaki wa Magufuli'

JAMHURI imeiomba Mahakama Kuu kutosikiliza maombi ya utetezi katika kesi ya kuvua samaki kwenye Bahari ya Hindi bila kibali, maarufu kama ‘Samaki wa Magufuli’ yaliyotaka kurejeshwa mali zilizokamatwa kwa madai kuwa mwombaji hana sifa.

Upande wa watoa maombi unataka mali hizo ambazo ni meli ya Tawariq 1 na zaidi ya Sh. bilioni mbili za tani 296.3 za samaki, zirejeshwe kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Sea Tawariq LLC, Said Ali Mohammed.

Hata hivyo, Jamuhuri inapinga ombi hilo ikidai kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, mali hizo zinatakiwa kukabidhiwa kwa mmiliki wa kampuni hiyo na siyo Mkurugenzi wake.

Wakili wa Serikali, Timon Vitalis, akitoa hoja zake jana mbele ya Jaji Ama-Isario Munisi, alisema:

"Mtukufu Jaji, haiwezekani maombi haya yaletwe katika mahakama hii kwa sababu Mahakama ya Kisutu ilishaamuru mali akabidhiwe mshtakiwa wa kwanza aliyekuwa kapteni wa meli hiyo."

“(Aidha) Mahakama ya Rufani ilishafuta mwenendo wa kesi ya msingi wa Mahakama Kuu kwa sababu hiyo, maombi haya ni batili hayawezi kusikilizwa na kutolewa amri mbili katika mahakama mbili zinazohusu kitu kimoja.

“Pia,mahakama hii haiwezi kuamuru mkurugenzi wa kampuni kurejeshewa mali hizo wanazodai utetezi kwa kuwa siyo kampuni.”

Wakili Vitalis aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) mahakamani hapo, alidai mkurugenzi ni mwajiriwa na siyo kampuni na kwamba kama upande wa utetezi wana hoja, wawasilishe katika mahakama iliyotoa amri hiyo.

Upande wa utetezi ulioongozwa na Mawakili Ibrahim Bendera na John Mapinduzi, ulidai waliwasilisha maombi hayo mahakamani hapo kwa sababu Mahakama ya Kisutu ilikataa kurejesha mali hizo kwa mshtakiwa wa kwanza.

Bendera alidai pia maombi hayo wamewasilisha mahakamani hapo kwa sababu vielelezo vilitolewa katika mahakama hiyo wakati wa usikilizwaji kesi ya msingi.

Jaji Munisi alisema baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, mahakama yake itatoa uamuzi Desemba 7.

Madai hayo yamewasilishwa Mahakama ya Kuu na raia wawili wa China, Hsu Tai na Zhao Hanquing ambao walikamatwa wakivua samaki katika Ukanda wa Kiuchumi wa Bahari ya Tanzania bila kibali.

Septemba Mosi, 2014 upande wa utetezi uliwasilisha barua ya maombi hayo mbele ya Msajili wa mahakama hiyo.

Katika barua hiyo, utetezi unaomba mahakama iwarejeshee vielelezo vilivyotolewa mahakamani wakati kesi namba 38 ya mwaka 2009 mbele ya Jaji Radhia Sheikh aliyeisikiliza.

Habari Kubwa