PM aagiza mashauri yote ya watoto yatolewe uamuzi ndani ya miezi 6

17May 2022
Paul Mabeja
DODOMA
Nipashe
PM aagiza mashauri yote ya watoto yatolewe uamuzi ndani ya miezi 6

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameviagiza vyombo vya sheria ikiwamo Jeshi la Polisi, Mahakama na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali (DPP), kufanyia kazi na kutoa uamuzi wa mashauri yote yanayohusu watoto ndani ya miezi sita na sio vinginevyo.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa.

Pia, amezionya familia ambazo zimekuwa na tabia ya kumaliza kesi zinazohusu watoto zenyewe bila kufikisha mashauri katika vyombo vya sheria kuacha mara moja.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera na Uratibu wa Bunge, George Simbachawene, alibainisha hayo juzi alipokuwa akifungua kongamano la kitaifa la malezi ya watoto na familia kwa niaba ya Waziri Mkuu.

“Waziri Mkuu amenituma nitoe maagizo haya kwa vyombo vyote vya sheria nchini kuhakikisha kuwa mashauri yote yanayohusu watoto yanafanyiwa kazi na kutolewa maamuzi ndani ya miezi sita na sio vinginevyo,” alisema Simbachawene.

Alisema hivi sasa matukio ya ukatili kwa watoto yamekuwa yakiongezeka na wahusika wakuu ni wanafamilia wenyewe.

Aidha, alisema jamii inapaswa kupaza sauti ili kupinga matukio ya ukatili kwa watoto kwa kuripoti katika vyombo vya sheria badala ya kumalizana kifamilia.

“Takwimu za Jeshi la Polisi zinaonyesha kuwa kuanzia Januari hadi Desemba, mwaka jana kesi za ukatili dhidi ya watoto zilizoripotiwa ni 11,499 ambapo matukio makubwa ni ubakaji 5,899, mimba 1,677 na ulawiti ni 1,114 na mengine mengi,” alisema Simabachawene.

Kadhalika, alisema kutokana na hali hiyo vyombo vyote vya ulinzi vinapaswa kushughulikia kwa haraka na kutolea uamuzi mashauri yote yanayohusu mimba kwa watoto, ubakaji pamoja na ulawiti.

“Pia wazazi wote ambao watabainika kumaliza wenyewe kwa wenyewe mashauri yanayohusu ukatili dhidi ya watoto kama vile ubakaji, ulawiti na mimba wachukuliwe hatua kali za kisheria ili iwe fundisho kwa wengine,” alisisitiza Simbachawene.

Vilevile, alisema moja ya sababu zinazochangia ongezeko la watoto wa mitaani ni migogoro katika familia inayosababisha ndoa kuvunjika na watoto kukosa malezi ya wazazi.

“Baadhi ya familia zinaishi bila upendo hali inayosababisha kutengana kwa wazazi na kusababisha ongezeko la watoto mitaani katika miji mbalimbali nchini, lakini serikali inaendelea kufanya jitihada za kumaliza hali hii ikiwamo ujenzi wa makao ya kulelea watoto nchini,” alisema Simbachawene.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, alisema serikali inatambua na inathamini familia kama chanzo cha nguvu kazi ya taifa.

“Hivyo katika kuimarisha uwezo wa familia kutimiza majukumu yake, serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, imekuwa ikitekeleza afua mbalimbali za kuwezesha familia kuishi kwa amani na upendo,” alisema Dk. Gwajima.

Alisema baadhi ya afua hizo ni kutoa elimu ya malezi chanya kwa wataalamu wa halmashauri 7,445 wakiwamo maofisa Maendeleo ya Jamii, Ustawi wa Jamii, Maofisa Lishe na walimu.

“Aidha, wataalamu hawa kwa kipindi cha Julai 2020 hadi Juni 2021 walifanikiwa kutoa mafunzo na wazazi na walezi vinara (Champion) 110,805 ambao wamepewa jukumu la kuendeleza elimu ya malezi kwa wenzao katika mikoa 26 ya Tanzania Bara.

Alisema Tanzania inaungana na nchi nyingine duniani katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Familia inayofanyika kila mwaka Mei 15.

Maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika kimkoa na mikoa yote 26 inafanya maadhimisho hayo kwa utaratibu ambao wanaona unafaa kulingana na mazingira yao.

Habari Kubwa