PM aagiza uchunguzi mil. 700/- za hospitali

19Nov 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
PM aagiza uchunguzi mil. 700/- za hospitali

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, aunde timu ya wataalamu kufuatilia Sh. milioni 700 zilizotolewa na serikali kukarabati Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea ambazo hadi sasa hazijatumika.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Walimu na baadhi ya wanafunzi wa Shule za Msingi za wilaya ya Ruangwa kwenye ukumbi wa Narung’ombe, Novemba 18, 2018. Kulia ni Mkewe Mary, kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi na wapili kulia ni Mkuu wa wilaya ya Ruangwa, Hashim Ngandirwa.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Kadhalika, Waziri Mkuu ameielekeza timu hiyo ikague matumizi ya Sh. milioni 400 zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ujenzi kituo cha afya cha kata ya Kilimarondo, ambazo zimeisha kabla ujenzi haujakamilika.

 

Alitoa maagizo hayo Jumamosi wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara kwenye kijiji cha Kilimarondo, Nachingwea mkoani Lindi, baada ya kukagua ujenzi wa kituo hicho cha afya.

 

“Serikali haitaki mzaha na fedha za umma, hivyo Mkuu wa Mkoa unda timu ya wataalamu kutoka mkoani waje Nachingwea kufuatilia ni kwa nini fedha zimetolewa tangu Julai ili kukarabati hospitali ya wilaya ziwe hazijatumika hadi leo. Pia tujue kama kweli bado zipo,” Mwaziri Mkuu aliagiza.

 

Waziri Mkuu alitoa agizo hilo baada ya Mbunge wa Nachingwea, Hassan Masala, kumweleza kwamba hadi sasa Sh. milioni 700 zilizotolewa na serikali Julai mwaka huu kwa ajili ya ukarabati wa hospitali ya wilaya hazijatumika.

 

Mbali na fedha hizo, pia mbunge huyo aliomba uchunguzi maalum ufanyike kwenye mradi wa ujenzi wa kituo cha afya cha Kilimarondo baada ya fedha zilizotolewa kumalizika bila  mradi kukamilika.

 

Mradi huo wa ujenzi wa kituo cha afya ulitengewa Sh. milioni 400 ambazo zimekwisha na zinahitajika Sh. milioni 51 kwa ajili ya kumalizia, ambapo Waziri Mkuu aliagiza halmashauri ihakikishe fedha hizo zinatolewa ili kukamilisha mradi huo.

 

Kukamilika kwa ujenzi wa kituo hicho cha afya kitakachokuwa kinatoa huduma mbalimbali zikiwamo za mama na mtoto na upasuaji kutawapunguzia wananchi kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 90 kutoka Kilimarondo hadi Nachingwea kufuata huduma za afya.

 

Kuhusu upatikanaji wa huduma ya nishati ya umeme, Waziri Mkuu alisema serikali imedhamiria kusambaza umeme katika maeneo yote ambavyo hayajaunganishiwa nishati hiyo yataunganishiwa, ikiwamo na tarafa ya Kilimarondo.

 

Waziri Mkuu alisema Rais John Magufuli anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inapata umeme tena kwa gharama nafuu na kuwa serikali imetenga fedha nyingi zitakazotosheleza kusambaza umeme katika maeneo yote kwa gharama ya Sh. 27,000 tu.

 

Pia Waziri Mkuu aliwaeleza wananchi hao kwamba hawatowajibika tena katika kulipia gharama za nguzo wala fomu za maombi ya kuunganishiwa umeme kwa sababu gharama hizo zimeshabebwa na serikali.

Katika hatua nyingine, Majaliwa alitembelea kituo cha afya cha Nkowe na kuwataka wananchi wakilinde na kukienzi kwa kuwa ndio mkombozi wao kiafya.Alisema hawana sababu ya kulipa nauli kwenda Ruangwa kufuata huduma za vipimo na matibabu katika hospitali ya wilaya hiyo.Waziri Mkuu alitembelea kituo hicho cha jana.Alitaja baadhi ya huduma zinazopatikana kwenye kituo hicho ambazo awali hazikuwapo ni upasuaji, maabara, mama na mtoto.Waziri Mkuu alisema amefurahishwa na huduma zinazotolewa kituoni hapo, ambapo aliwataka watumishi waendelee kuwahudumia wananchi vizuri.Baadhi ya wagonjwa waliolazwa katika kituo hicho waliishukuru serikali kwa kuboresha huduma za afya nchini, ambapo kwa sasa wanatibiwa karibu na makazi yao. Awali, Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dk. Paul Mbinga, alisema kituo hiko kinahudumia jumla ya wakazi 5,264 wa Kata ya Nkowe na wa kata za jirani za Chienjele, Nandagala, Likunja na Mnacho. Alisema baada ya kukamilika kwa mradi huo wananchi sasa wanapata huduma ambazo walikuwa wanalazimika kuzifuata katika hospitali ya wilaya zikiwamo za upasuaji, damu salama, maabara, kujifungua, kulaza wagonjwa na kuhifadhi maiti.Dk. Mbinga alisema mradi wa ujenzi wa kituo hicho uliogharimu Sh. milioni 500 umepunguza gharama kwa wananchi zinazoambatana kwenda kutibiwa katika hospitali ya wilaya ambayo ipo umbali wa kilomita 20. Baada ya Waziri Mkuu kutembelea kituo, alikwenda kukagua ujenzi wa Gereza la Wilaya ya Ruangwa na mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi ya askari magereza wa gereza hilo.

Habari Kubwa