PM aagiza uwezeshaji watafiti wa michikichi

18Feb 2019
Na Mwandishi Wetu
Kigoma
Nipashe
PM aagiza uwezeshaji watafiti wa michikichi

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameiagiza Wizara ya Kilimo iwawezeshe watafiti katika kituo cha utafiti cha zao la michikichi cha Kihinga mkoani Kigoma, ili waongeze kasi ya uzalishaji wa mbegu bora za zao hilo.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, picha mtandao

Alisema serikali imeamua kuongeza nguvu kwenye michikichi, hivyo Wizara ya Kilimo hainabudi kukiwezesha kituo hicho kwa lengo la kuzalisha mbegu bora zitakazosambazwa kwa wakulima.

Waziri Mkuu alitoa maagizo hayo jana alipotembelea kituo cha Kihinga kwa ajili ya kukagua shughuli za uzalishaji wa mbegu za michikichi, akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Kigoma.

Alisema serikali imeamua kulifufua zao hilo kwa lengo la kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini, ambapo kwa mwaka inatumia zaidi ya Sh. bilioni 600 kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi.

“Wizara ya Kilimo iwawezeshe watu wa utafiti ili waendelee na shughuli hiyo kwa kasi, iwaongeze watumishi kituoni hapa na ongezeni nguvu kwenye zao la michikichi kama yalivyofanya mataifa mengine ya Costa Rica na Malaysia.”

Alisema wakulima wa zao hilo wanahitaji kupata mafanikio, hivyo kituo hakinabudi kuongeza nguvu ya uzalishaji wa mbegu bora, ili wafikie malengo aliwashauri washirikiane na taasisi binafsi zinazozalisha mbegu.

Pia, Waziri Mkuu alisema Chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Kihinga, kiendelee kutoa elimu na Wizara ya Kilimo ijenge majengo yake inayoyahitaji kwa ajili ya kufanyia shughuli za utafiti.

Mratibu wa Utafiti wa Kilimo kwa mikoa ya Tabora na Kigoma, Dk. Filson Kagimbo, alisema michikichi iliyopo sasa ina uwezo wa kuzalisha tani 1.6 ya mawese kwa hekta moja ambao kidogo na hauna tija.

Alisema mbegu wanazozizalisha zinalenga kumuongeza tija mkulima kwa kuwa zitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani nne kwa hekta, pia wanaendelea kuangalia vinasaba vya mbegu vilivyopo ili wazalishe mbegu bora zaidi.

“Tutakusanya vinasaba vyote vya mbegu tulivyonavyo na kuvitathmini na kuona uwezo wake na ikibidi tutaagiza kutoka nje ya nchi ili kuboresha zaidi.” Miche ya michikichi inachukua muda wa miezi 18 kutoka hatua ya uchavushaji hadi kusambazwa kwa wakulima.

Baada ya kumaliza shughuli ya ukaguaji wa uzalishaji wa mbegu kituoni hapo, Majaliwa alikagua shamba la michikichi la Gereza la Kwitanga lenye ukubwa wa ekari 400 na kupanda mche kama ishara ya uzinduzi wa upandaji wa miche bora shambani hapo.

Waziri Mkuu amesema Serikali imeamua kuongeza nguvu katika zao hilo na inategemea taasisi zake mbili za Jeshi la Magereza (Kwitanga) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT-Bulombora), ambazo zina mashamba makubwa ya michikichi.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliagiza elimu kuhusu kilimo cha michikichi kuanzia hatua za awali hadi uzalishaji wa mafuta itolewe mashuleni ili wanafunzi waanze kupata ulewa na ifikishwe hadi kwa wananchi.

Habari Kubwa