PM aipa neno KKKT ukamilishaji chuo SEKOMU

17Jan 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
PM aipa neno KKKT ukamilishaji chuo SEKOMU

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameutaka uongozi mpya wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki inayomiliki chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (SEKOMU), ukamilishe mahitaji ambayo yataiwezesha Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

Alitoa kauli hiyo jana wakati alipokutana Askofu Mteule wa Dayosisi hiyo Mchungaji Dk. Msafiri Mbilu pamoja na viongozi wengine wapya waliochaguliwa. Kikao hicho kilifanyika katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Mlimwa.

Waziri Mkuu alisema hayo baada ya Askofu Dk. Mbilu kuiomba serikali iusaidie uongozi wa Dayosisi hiyo kukiwezesha chuo hicho kufunguliwa na kuruhusiwa kufanya udahili. Mwaka 2018 TCU ilikisitishia chuo hicho kufanya masomo na udahili wa wanafunzi katika ngazi zote baada ya kukosa vigezo.

“Kamilisheni mahitaji yatakayokifanya chuo chenu kiweze kuendelea kufanya udahili. Taarifa niliyonayo ni kwamba TCU walishakuja kukutana nanyi na kufanya ukaguzi, walitoa mahitaji kadhaa ambayo mnapaswa kuyakamilisha na nimesikia mmeridhia na kazi hiyo inaendelea.”

Mbali na agizo hilo, pia Waziri Mkuu aliwashukuru viongozi wa dini nchini kutokana na mchango mkubwa wanaoendelea kuutoa kwa taifa. “Viongozi wa dini ni watu muhimu sana, nchi imetulia na ina amani, hivyo kuwa kimbilio kwa waliokosa amani makwao.”

Awali, Askofu Dk. Mbilu alimweleza Waziri Mkuu kwamba Chuo Kikuu cha SEKOMU kimezuiliwa kufanya udahili kutokana na changamoto mbalimbali za kimfumo wa ndani ya Dayosisi na ndani ya chuo ikiwa ni pamoja na kuwa na viongozi wa kukaimu kwa muda mrefu jambo ambalo kwa sasa tayari limeshapatiwa ufumbuzi.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni madeni makubwa yakiwamo ya mishahara ya watumishi, ambayo tayari uongozi umeshaanza kulipa malimbikizo hayo na wameweka mipango ya kumaliza kulipa madeni hayo. Pia, kiongozi huyo alisema chuo kimeshapata walimu wa kutosha chuo kitakapofunguliwa....soma zaidi kupitia https://epaper.ippmedia.com

Habari Kubwa