PM asema changamoto za mkonge kutatuliwa

23Jan 2021
Na Mwandishi Wetu
Tanga
Nipashe
PM asema changamoto za mkonge kutatuliwa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema serikali itahakikisha changamoto zote zilizokuwa zinawakabili wakulima wa mkonge, ikiwamo kuibiwa mapato hazijirudii.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, picha mtandao

Aliyasema hayo juzi alipozungumza na wananchi baada ya kukagua shamba la mkulima mdogo lililoko Magunga Estate wilayani Korogwe.
                                                                                                                     
Waziri Mkuu alisema miaka ya nyuma Tanzania ilikuwa inashika nafasi ya pili duniani katika kilimo cha mkonge kwa kuzalisha tani 200,000 kwa mwaka ikitanguliwa na Brazil.

Hata hivyo, alisema uzalishaji wa zao hilo ulishuka kutoka tani 200,000 kwa mwaka na hadi tani 39,000 na sasa serikali imedhamiria kuongeza uzalishaji na kufikia tani 150,000 ifikapo 2025.
 
“Awali wakulima walikuwa wanaibiwa sana jambo ambalo kwa sasa halitojirudia tena kwani serikali imejipanga ipasavyo kuhakikisha mkulima ananufaika, hivyo tulime mkonge unalipa,” alisema.
 
Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigela, alisema awali wakulima wa mkonge walikuwa wakilipwa Sh. 50,000 kwa tani kutokana na kuibiwa na watu wasio waaminifu, lakini baada ya serikali kuingilia kati, bei imeongezeka hadi Sh. milioni nne.

Shigela alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya serikali kuamua kusimamia mwenendo wa biashara ya kilimo cha mkonge na tayari wakulima wameanza kupata tija.
 
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge, Saady Kambona, alisema wamepokea zaidi ya maombi 2,000 ya wananchi wanaohitaji mashamba kulima mkonge.
 
Alisema Bodi imepeleka maombi Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kurudishiwa mashamba ambayo yametelekezwa ili wayagawe kwa wananchi.
 
Kambona alisema kwa sasa hamasa ya kilimo cha mkonge ni kubwa baada ya serikali kuonyesha dhamira ya kulifufua zao hilo na wananchi wengi wamejitokeza wameomba mashamba.
 
Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) cha Magunga, Shedrack Lugendo, alisema uzalishaji wa mkonge umekuwa mzuri baada ya chama chao kusimamia na Desemba, mwaka jana, walipata daraja la juu ambalo ni 3L kiasi cha tani mbili baada ya kupita miaka 10.
 
Kuhusu shamba la mkulima mdogo, Estohim Urio, ambalo Waziri Mkuu alilitembelea, alisema mkulima huyo anamiliki hekta 200 alizopewa na Bodi ya Mkonge.
 
Mwenyekiti huyo alisema mkulima huyo amepanda hekta 182 ambazo mkonge mkubwa unaovunwa ni hekta 113 na eneo lenye mkonge mdogo ni hekta 69.
 

Habari Kubwa