PM asema kilimo bado kina nafasi mageuzi ya kiuchumi

20Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Mwanza
Nipashe
PM asema kilimo bado kina nafasi mageuzi ya kiuchumi

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema sekta ya kilimo ina nafasi kubwa ya kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini iwapo changamoto zinazoikabili zikiwamo upatikanaji wa pembejeo, mbinu na miundombinu duni ya uzalishaji, usafirishaji, uchakataji wa mazao na masoko zitafanyiwa kazi kwa wakati. 

Majaliwa aliyasema hayo jana wakati akifungua ofisi za Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa Kanda ya Ziwa na kuutaka uongozi wa benki hiyo ushirikiane na wadau wengine kutatua changamoto hizo.

Alisema bado sekta za kilimo, mifugo na uvuvi zimeendelea kukabiliwa na changamoto nyingi ambazo kwa kiasi kikubwa zimesababisha tija ndogo hususan kwa wakulima wadogo.

Kutokana na hali hiyo, aliwaagiza viongozi wa TADB kuendeleza kasi ya utoaji huduma ili kuwafikia wakulima na wafuaji wengi zaidi nchini.

“Endeleeni kufanya kazi na wadau mbalimbali kwa ajili ya kuweka na kutekeleza mipango ya utatuzi wa changamoto zinazowakabili wakulima, wafugaji na wavuvi nchini. Pia panueni zaidi wigo wa huduma hususan utoaji wa mikopo katika kuendeleza miradi ya miundombinu ya kilimo, ufugaji na uvuvi na kutoa mafunzo kwa wakulima wadogo kwa lengo la kuinua uzalishaji,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alisema kwa kuwa Benki Kuu ndiyo mdhibiti mkuu wa benki zote nchini, hivyo inao wajibu wa kutambua umuhimu wa kuandaa kanuni mbadala na sera za fedha ambazo ni rafiki kwa benki za maendeleo ya kilimo na ujasiriamali. 

Alisema lengo ni kurahisisha utoaji wa huduma ya mikopo ya kibiashara tena yenye kuvutia kwenye sekta ya kilimo, hivyo akaitaka Benki Kuu iangalie namna ya kushirikiana na wadau hususan wa kilimo kuandaa kanuni maalumu za usimamizi angalifu wa fedha ambazo zitazingatia mazingira halisi ya kilimo na changamoto zake.

“Sambamba na kushughulikia sera au kanuni ambazo zinarahisisha kufanya biashara katika kilimo. Benki Kuu pia inatakiwa kuendesha kazi hiyo bila kuhatarisha utulivu wa kifedha na kujihami na madhara na hatari zinazoambatana na ukopeshaji,” alisema.

Naye Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bushungwa, alisema ufunguzi wa benki hiyo kwa Kanda ya Ziwa ni hatua nzuri ambayo inakwenda kuwasogezea huduma wakulima, hivyo ameutaka uongozi wa benki hiyo uandae utaratibu wakuwafundisha wakulima namna ya kuandika maandiko kwa ajili ya kuomba mikopo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Japhet Justine, alisema hadi Februari 28, mwaka huu benki ya TADB imekuza mtaji wake na kufikia Sh. bilioni 68 ikiwa ni ongezeko la asilimia 13 kutoka mtaji wa Sh. bilioni 60 uliotolewa na serikali mwaka 2015.

Mkurugenzi huyo alisema ukuaji wa mtaji wa benki hiyo umechangiwa na malimbikizo ya faida iliyotengenezwa katika kila mwaka wa fedha tangu kuanzishwa kwa benki hiyo mwaka 2015, kutokana na utoaji wa mikopo ya kimkakati inayotolewa kwa wateja wao.

Habari Kubwa