PM asisitiza umuhimu mifumo usalama mijini kupitia TEHAMA

25Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
PM asisitiza umuhimu mifumo usalama mijini kupitia TEHAMA

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema serikali imetenga shilingi bilioni 170 kwa ajili ya ujenzi wa Mkongo wa Taifa katika mwaka wa fedha 2021/2022, huku akisisitiza umuhimu wa mifumo ya usalama kupitia TEHAMA katika miji mbalimbali nchini.

Majaliwa ameyasema mwishoni mwa wiki  alipofungua Mkutano wa Tano wa Mwaka wa TEHAMA Tanzania uliofanyika jijini Arusha.

Kuhusu Mkongo wa Taifa, fedha hizo zitawezesha kujenga kilomita 4,244 za mkongo huo ili kufikisha jumla ya kilomita 12,563.

“Lengo letu ni kuwawezesha watoa huduma za mawasiliano kutumia miundombinu hii kuboresha huduma za mawasiliano nchini na kurahisisha ufikishwaji wa intaneti kwenye ofisi mbalimbali za sekta ya umma na binafsi,” alisema.

Majaliwa aliiagiza Wizara ya Habari, Sayansi na Teknolojia ya Habari isimamie kwa karibu mradi wa upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili wananchi wengi zaidi washiriki katika ujenzi wa uchumi wa kidijitali.

“Hivi sasa serikali imejenga kilomita 8,319 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano hadi Septemba 2021. Malengo yetu kama serikali ni kujenga hadi kilomita 15,000 ifikapo mwaka 2024/2025. Hili linahitaji uwekezaji mkubwa na serikali imejipanga kuwekeza vilivyo, lakini tunakaribisha wabia na wawekezaji katika eneo hili pamoja na maeneo mengine ya TEHAMA,” alisema.

Kuhusu umuhimu wa uwapo wa mifumo ya usalama kupitia TEHAMA katika miji mbalimbali nchini, alisema zitasaidia kuongeza usalama kwa kuwa utawezesha kuwa na rekodi za matukio mbalimbali yakiwamo yakihalifu katika maeneo hayo.

“Nilipata nafasi ya kufanya ziara China na nikatembelea ilipo kampuni ya Huawei, hapo nilijionea teknolojia kubwa na za kisasa ambazo tunaweza kuzitumia hapa nchini pia,” alisema Waziri Mkuu.

Baada ya kufungua mkutano huo, Majaliwa pia alizindua mwongozo wa usajili wa wataalamu wa TEHAMA na kutoa vyeti kwa baadhi ya wataalamu wa TEHAMA ambao wamesajiliwa.

Waziri wa Habari, Sayansi na Teknolojia ya Habari, Dk. Ashatu Kijaji, alisema wizara yake imejipanga kujenga kituo mahiri cha kukuza utaalamu na utafiti nchini ambacho kitajengwa jijini Dodoma kwa kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali “Digital Tanzania.”

Miongoni mwa waliotunukiwa tuzo ni pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kulibeba suala la TEHAMA kwa nguvu zake zote na kuliweka kwenye vipaumbele vya serikali.

Awali, katika mahojiano yake na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huawei Tanzania, Damon Zhang, alisema kampuni hiyo ipo tayari na imejitolea kufanya kazi na serikali katika kuleta maono ya pamoja ya kukuza uchumi wa kidijiti, sambamba na kudhibiti changamoto zilizoletwa na ustawi wa TEHAMA.

“Tunajitolea kuendelea kukuza ujumuishaji wa kidijiti kwa kila mtu, kila nyumba, na kila shirika kwa ajili ya kuandaa Tanzania iliyounganishwa,” alisema.

Habari Kubwa