PM ataka kasi kanuni masoko ya madini

27Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
PM ataka kasi kanuni masoko ya madini

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa, ameiagiza Wizara ya Madini kukamilisha kanuni za uendeshaji wa masoko ya madini katika mikoa yote nchini na kuanza kutumika kwa wakati ili kuongeza tija kwenye sekta hiyo.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa

Katika kukabiliana na changamoto ya utoroshwaji wa madini nchini, Rais John Magufuli aliagiza kuanzishwa kwa masoko ya madini kwenye mikoa yote, hivyo Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Madini na wakuu wote wa mikoa watekeleze maagizo hayo haraka.

 

Majaliwa aliyasema hayo jana wakati akifungua mkutano kuhusu uanzishwaji wa masoko ya madini katika mikoa yote nchini. Mkutano huo ulifanyika kwenye ukumbi wa Kambarage, Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dodoma.

 

Mkutano huo wa wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa, ulihudhuriwa na mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu na manaibu makatibu wakuu na watendaji wa Wizara ya Madini na wa Tume ya Madini.

 

Waziri Mkuu alisema katika kuanzishwa kwa masoko hayo, rasimu ya kanuni imeandaliwa, hivyo ni vyema wakazielewa vizuri kwa sababu wao ndio watakaozitekeleza kwenye maeneo yao ili serikali ifikie lengo ililojiwekea katika kuimarisha sekta ya madini.

 

”Kutokana na umuhimu wa masoko hayo, naagiza kanuni hizo zikamilishwe haraka iwezekanavyo ili kuwasaidia watu wetu kupata masoko ya uhakika ya madini na serikali itanufaika na mrabaha na tozo mbalimbali zitakazokuwa zikitozwa kwa mujibu wa sheria,” alisema.

 

Pia aliagiza pindi kanuni hizo zitakapokamilika, Wizara ya Madini ihakikishe zinafikishwa kwa wakurugenzi wa majiji, manispaa na halmashauri za wilaya, maeneo ya machimbo, wachimbaji na wafanyabiashara wa madini ili kuondoa migogoro.

 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka wakuu wa mikoa kusimamia kikamilifu ulinzi na usalama kwenye masoko hayo ili kuwahakikishia wafanyabiashara, wachimbaji na wananchi usalama wa kutosha wakati wa kuuza madini.

 

Alisema kwa muda mrefu Rais Magufuli amekuwa akisisitiza kuhusu sekta ya madini kuchangia ipasavyo katika pato la taifa,  hivyo kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijami kwa wananchi, lakini imekuwa na matatizo ikiwamo utoroshwaji wa madini na migogoro kwa wachimbaji hususani wachimbaji wadogo.

 

”Jitihada mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa kuhakikisha changamoto hizo zinaondolewa kwa lengo la kuongeza tija kwenye sekta ya madini. Napenda mfahamu kuwa mna nafasi muhimu katika kuifanya sekta hii iweze kuleta manufaa yanayotarajiwa kwa Taifa, alisema.”

 

Waziri wa Madini, Doto Biteko, alisema mkutano muhimu kwa sababu unalenga kumaliza changamoto ya masoko ya madini nchini, hivyo amewataka wakuu wa mikoa wahakikisha wanalipa kipaumbele jambo hilo kwa kuwa linamanufaa kwa Taifa.

 

Alisema kwa sasa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini hawana maeneo maalum wanayoweza kufanyia biashara ya madini hali ambayo inachangia kuwapo kwa utoroshwaji wa madini, jambo ambalo linasababisha serikali kukosa mapato.

 

 

Habari Kubwa