PM ataka Watanzania kuendelea kushikamana

24Feb 2021
Na Mwandishi Wetu
Mtwara
Nipashe
PM ataka Watanzania kuendelea kushikamana

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewataka Watanzania waendelee kushikamana katika kipindi hiki ambacho dunia ina mahangaiko makubwa na magonjwa mbalimbali ya maambukizi.

”Tuendelee kumtegemea Mwenyezi Mungu kama Mheshimiwa Rais Dk. John Magufuli alivyotusisitiza na tuendelee kuiamini serikali na jitihada za viongozi wake tutapata utulivu.”

Waziri Mkuu aliyasema hayo, juzi, aliposhiriki mazishi ya mfanyabiashara maarufu katika mikoa ya Lindi na Mtwara, Ally Nalaga, yaliyofanyika Mnazimmoja Lindi.

Alisema magonjwa hayo yameleta tafsiri tofauti na wakati mwingine kutokuwa na utulivu, kwani watu wanatishana sana, hali ambayo inawafanya wasiwe na amani na kuwajengea hofu.

Waziri Mkuu alisema serikali inaendelea kufuatilia mwenendo wa aina zote za magonjwa ambayo yanawakabili wananchi katika maeneo mbalimbali nchini na kuyatafutia tiba.

Hata hivyo, Waziri Mkuu aliwasisitiza wananchi waendelee kuchukua tahadhari ya kila ugonjwa. ”Ukisikia Ukimwi kuna tahadhari zake, ukisikia kipindupindu kina tahadhari zake.”

Pia Waziri Mkuu aliwaomba viongozi wa dini zote nchini waendelee kuliombea Taifa na viongozi ili liendelee kuwa na amani na kimbilio kwa walipoteza amani.

Akimzungumzia  marehemu Nalaga, Waziri Mkuu alisema alikuwa mcheshi na mwenye upendo kwa kila mtu na alijitoa sana katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya jamii.

”Tumepoteza mtu muhimu kwenye jamii yetu ya wana Lindi na Mtwara. Nalaga ametuachia mambo mengi, hivyo tumuombea kwa Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema.”

Habari Kubwa