PM awafunda maofisa habari

19Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe
PM awafunda maofisa habari

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amewataka maofisa habari, uhusiano na mawasiliano serikalini kujitathmini kuhusu walivyotekeleza wajibu wao na kutafakari njia bora ya kuyatangaza na kuyatetea mafanikio ya mageuzi yanayoendelea nchini.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, picha mtandao

Pia, aliwataka kuhakikisha wanatumia vizuri taaluma zao na nyenzo wanazopatiwa kusema mambo yanayofanywa kwenye sekta zote ili kuepuka upotoshaji kwa wapinga maendeleo.

Aliyasema hayo jana, katika ufunguzi wa kikao kazi cha 15 cha maofisa hao, kinachofanyika jijini Mwanza na kuhudhuriwa na maofisa hao wapatao 400.

Aliwataka maofisa hao kuueleza umma masuala yanayofanywa na serikali hususan katika kipindi hiki ambacho serikali inatekeleza Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2016/2017 – 2020/2021), wenye kuweka msisitizo kwenye ujenzi wa uchumi wa viwanda.

"Mkumbuke kuwa kazi ya utoaji taarifa kwa wananchi kwa sasa si utashi binafsi wa mtoa habari, bali kufanywa kwa mujibu wa sheria na Katiba ya nchi. Mathalan Sheria mpya ya Haki ya Kupata Taarifa Na. 12 ya mwaka 2016, yenye kuzitaka mamlaka za umma kuwapa wananchi taarifa zinazowahusu," Waziri Mkuu alisema.

Alisema sheria hiyo, inaendana na sheria nyingine ya kumlinda mwananchi asilishwe taarifa za uongo, uchochezi na uzushi yaani Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari Na. 12 ya mwaka 2016.

Alisema lengo la katiba na sheria hizo mbili, ni kuwahakikishia wananchi haki ya kupata habari zilizothibitishwa kwa maana ya usahihi na kwa wakati. "Sababu hizo, ndizo zilizofanya niguswe sana na kaulimbiu yenu isemayo: "Utoaji habari sahihi na kwa wakati ni chachu katika kuifikia Tanzania ya kipato cha kati".

Aidha, Waziri Mkuu alipongeza kazi zinazofanywa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo (hususan Idara yake ya Habari - MAELEZO) na timu za habari za viongozi wakuu kama mawaziri, wakuu wa mikoa na watendaji wengine.

Alisema ameguswa na baadhi ya mada zitakazojadiliwa katika kikao kazi hicho, ikiwamo ya namna ya kushughulikia habari za uongo, kutunga, kughushi na namna kada yao inavyoweza kusaidia kukidhibiti kichochoro hicho haramu katika habari.

Aliwataka viongozi na watendaji wote wa taasisi za umma, kuanzia sasa washirikiane na maofisa wa habari kwenye maeneo yao kuhakikisha habari muhimu kwa wananchi hazizuiwi kwa urasimu kama hazijazuiwa kisheria. Habari zitolewe kwa haraka na kwa njia anuai za kisasa.

Alimwagiza Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, afuatilie uzinduzi wa tovuti za halmashauri walioufanya jijini Dodoma Machi 27, 2017, kama zinafanya kazi ipasavyo.

Alisema lengo la tovuti hizo ni kuiongezea serikali uwezo wa kuwapatia wananchi habari na taarifa kwa haraka kwa kuzingatia wako katika kipindi muhimu cha mageuzi katika historia ya nchi na mambo mengi yanafanyika serikalini ya kiuchumi na kijamii, lakini hayafikishwi kwa wananchi.

"Kuhusu hili, naiagiza Wizara ya Habari kufanya tathmini ya mara kwa mara na kuniletea taarifa kuhusu utekelezaji wa majukumu yenu na matakwa haya ya kisheria miongoni mwa wizara, taasisi za umma na sekretarieti za mikoa na halmashauri mbalimbali nchini."

Waziri Mkuu ametaja mapinduzi makubwa yaliyofanyika kwenye kila sekta nchini ikiwamo elimu; afya; nishati; mifugo; viwanda;
barabara; viwanja vya ndege; uchukuzi wa anga; uchukuzi wa reli; uchukuzi wa majini; madini; sanaa za filamu na muziki; utalii na michezo mbalimbali na kuwataka maofisa hao kutangaza mageuzi hayo

Habari Kubwa