PM: Tutakuza uchumi wa mtu mmoja mmoja

21Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
PM: Tutakuza uchumi wa mtu mmoja mmoja

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amesema mkakati wa serikali ya awamu ya sita ni kuboresha na kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja, hivyo kila Mtanzania afanye kazi kwa bidii.

“Sasa tunakwenda kusimamia maboresho ya uchumi wa mtu mmoja mmoja, Watanzania wote kila mmoja katika eneo la migodini, viwandani, wavuvi, wakulima, wasomi na wafanyabiashara wafanye kazi kwa bidii ili kujiongezea tija.”

Ameyasema hayo juzi wakati akizungumza na wananchi, baada ya kukagua ujenzi na ukarabati wa miundombinu katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kilichoko wilayani Karagwe, mkoani Kagera akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa huo.

Majaliwa alisema katika kuhakikisha mkakati huo unafanikiwa, Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya VETA katika kila halmashauri. Vyuo hivyo vinatoa mafunzo mbalimbali yatakayowawezesha vijana hao kujiajiri au kuajiriwa.

Alisema mafunzo hayo ambayo yatakuwa yanatolewa katika taaluma za TEHAMA, ufundi umeme, makenika, ushonaji nguo, utawawezesha vijana wa Kitanzania kujiajiri au kuajiriwa. “Hatua hii itawakwamua kiuchumi na kuwaondoa katika utegemezi, huu ndio mkakati wa Rais Samia.”

Hata hivyo, Majaliwa ameonyesha kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi huo ambao unagharimu shilingi bilioni sita na kumuagiza mkandarasi anayenga ambaye ni Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ahakikishe anaukamilisha kwa wakati ili malengo ya serikali yaweze kutimia.

Mradi huo unahusisha ukarabati majengo matano na kujenga majengo mapya manane ambayo ni kubadilisha jengo la utawala kuwa madarasa, kukarabati karakana ya ushonaji, kubadilisha jengo la bohari na kuwa karakana ya ufundi wa zana za kilimo na ufundi bomba.

Pia, kubadilisha bohari ya vitu vya jumla kuwa karakana ya uchomeleaji na uungaji vyuma kukarabati karakana ya ufundi wa magari.