Polepole na Gwajima wawekwa kiporo CCM

19Dec 2021
Paul Mabeja
Dodoma
Nipashe Jumapili
Polepole na Gwajima wawekwa kiporo CCM

​​​​​​​HATMA ya wabunge Humphrey Polepole, Jerry Silaa na Askofu Josephat Gwajima iko mikononi mwa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa baada ya taarifa ya Kamati ya Maadili ya Wabunge kutua mbele ya kamati hiyo.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi CCM, Rais Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Dk. Philip Mpango nje ya Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma baada ya kumalizika kwa Kikao cha Kawaida cha Halmashauri Kuu ya Taifa jana. PICHA: IKULU

Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, alibainisha hayo jana jijini Dodoma alipotoa taarifa ya kikao cha Halmashauri Kuu ya chama hicho kwa waandishi wa habari.

Shaka alisema wabunge hao watatu wataitwa kwenye Kamati Kuu ya chama hicho ili kupatiwa haki yao ya msingi na kikatiba ya kusikilizwa.

"Tayari taarifa ya Kamati ya Maadili ya Wabunge wa CCM na ile ya bunge ipo Kamati Kuu na wabunge hawa watatu wataitwa ili kupatiwa haki yao ya msingi ya kujieleza katika siku ambayo itapangwa na Kamati Kuu," alisema Shaka.

Mbunge wa Kawe, Gwajima, Mbunge wa Ukonga, Silaa na Mbunge wa Kuteuliwa, Polepole, hivi karibuni wametuhumiwa kuwa na mienendo ya kitabia isiyofaa ndani ya chama hicho.

Akizungumzia mambo mengine yaliyojadiliwa katika kikao hicho, Shaka alisema hoja kuu zilikuwa ni pamoja na kutoa pongezi kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri anayoifanya katika kusimamia utekelezaji wa ilani ya chama.

“Rais anasimamia ilani katika masuala ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Rais Samia ameweza kutatua kero na changomto za wananchi katika masuala ya huduma za maji, afya na umeme," alisema.

Shaka alisema kuwa kisiasa, Rais yuko tayari kuunganisha nchi na kwa kulithibitisha hilo hivi karibuni alishiriki mkutano wa wadau wa masuala ya demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini.

Katibu huyo pia alizungumzia maandalizi ya maadhimisho ya miaka 45 ya kuzaliwa kwa CCM yatakayofanyika Februari mwakani, akisema chama hicho kimerudisha utaratibu wa zamani wa maadhimisho ya kitaifa ambapo uzinduzi wake utafanyika Kusini Unguja Januari 19, 2022 na kilele chake ni Februari 5 mwakani mkoani Mara.

"Maadhimisho hayo ya kuzaliwa kwa CCM yataambatana na shughuli mbalimbali ikiwamo matembezi ya mshikamano na kutafakari uchaguzi wa ndani ya chama ambao unatarajiwa kufanyika mwakani pamoja na kutafakari Azimio la Arusha linalosisitiza uongozi bora na siasa safi," alisema.

Shaka alisema chama kinatoa shukrani kwa wanachama wake kwa kuwa pamoja katika kuwaunga mkono viongozi wakuu wa chama.

Habari Kubwa