Polepole ashauri umakini uhamishaji machinga

21Sep 2021
Enock Charles
DAR ES SALAAM
Nipashe
Polepole ashauri umakini uhamishaji machinga

MBUNGE Humphrey Polepole ameshauri kuwapo kwa umakini katika suala la kuwahamisha wafanyabiashara wadogo maarufu ‘Machinga’ katika maeneo ya barabarani.

Amesema lazima kwanza ijulikane hatima ya watakapopelekwa kwa kufanya uchambuzi wa kina.

Akizungumza katika darasa lake la mtandaoni, Polepole ambaye aliwahi kuwa Katibu Mwenezi wa CCM Taifa, alisema ni vyema kuzingatia uchambuzi wa wadau kuhusu uhakika wa soko katika maeneo watakapowahamishia machinga.

“Kuhusu habari ya wamachinga tuwe ‘very carefully’ (makini) na hii ‘issue’ (suala) kwa sababu ukikurupuka tu na hii issue inakwenda vibaya lazima tu ‘apply’ sayansi kwenye jambo hili kwa nini watu wapo barabarani kwa mfano usiwahamishe mpaka wamekujibu kwanini wapo barabarani, hapa nazungumzia uchambuzi wa wadau,” alisema Polepole.

“Halafu waulize eti nikikutengenezea soko mahali fulani utakwenda au huendi atakupa sababu za kwenda atakupa kwa maana ya zile nzuri na mbaya halafu wewe utaangalia je inawezekana kumpeleka kule sasa kwa mazingira ya sasa hivi,” alisema.

Wiki iliyopita Rais Samia Suluhu akiwaapisha mawaziri Ikulu, jijini Dodoma aliagiza wakuu wa wilaya na mikoa nchini kuwapanga vyema na kuonya anayoyaona kwenye runinga ya ngumi, kupigana, kufukuzana, kuchafuliana na vitu kumwagwa, hataki kuyaona.

“Niwaombe sana ndugu zangu wakuu wa mikoa mnaonisikia na wale wanaonisikia kupitia runinga wachukue hatua zinazostahiki bila kuleta vurugu, fujo na uonevu,” alisema.

Alitoa wito kwa machinga au wajasiriamali wafuate sheria na kanuni zilizopo na wajitahidi kufuata yale wanayopangiwa na wakuu wa mikoa na wilaya.

Tayari katika Jiji la Dar es Salaam mabango ya kutangaza kuwaondoa machinga walioweka vibanda juu ya mifereji ya maji, njia za wapita kwa miguu, hifadhi za barabara na mbele ya maeneo ya taasisi za umma kama shuleni yamewekwa ili kutoa tahadhari kwa wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika maeneo hayo.

Habari Kubwa