Polepole awaita Chadema wakorofi

19Feb 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Polepole awaita Chadema wakorofi

SIKU chache baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kutoa maazimio ya kufanya mikutano ya hadhara nchi nzima, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, amedai hatua hiyo ni ukorofi na uvunjifu wa sheria.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, picha mtandao


Wiki iliyopita, Chadema kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Dk. Vincent Mashinji, ilitangaza kuwa Kamati Kuu ya chama hicho imeamua waanze kufanya mikutano ya hadhara nchi nzima licha ya kuwapo kwa zuio la serikali kufanya mikutano hiyo na maandamano.


Dk. Mashinji alisema licha ya kuwapo kwa zuio hilo, CCM kimekuwa kikifanya mikutano ya hadhara maeneo mbalimbali nchini, akitolea mfano mikutano ya aina hiyo iliyofanyika hivi karibuni Karatu na Arumeru.


Akizungumza na Nipashe jana, Polepole alidai CCM haijawahi kufanya mikutano ya hadhara tangu kutolewa kwa zuio la mikutano hiyo.


Alisema kuwa kama Chadema wameamua kufanya mikutano ya hadhara, wasitafute kisingizio kwamba CCM inafanya mikutano ya aina hiyo. Alidai CCM inafanya mikutano ya ndani.

"Unajua mtu mkorofi ni mkorofi tu. Nimemsikia Katibu Mkuu wa Chadema (Dk. Mashinji) anasema sisi (CCM) tunafanya mikutano ya hadhara. Sisi tunafanya mikutano ya ndani, mimi nimekwenda Karatu, CCM tuna ofisi yenye uwanja mkubwa na kuna geti na maeneo mengine Arusha, Meru, Longido kote nimefanya mikutano ya ndani," Polepole alisema.


Juni 23, 2016, Rais John Magufuli alitangaza kupiga marufuku vyama kufanya mikutano ya siasa mpaka baada ya miaka mitano ili wananchi wahoji wanasiasa kama wametekeleza yale waliyoyaahidi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.


Alitoa kauli hiyo Ikulu Dar es Salaam baada ya kukabidhiwa ripoti ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damian Lubuva.


"Niwaombe wanasiasa wenzangu, wafanye siasa za ushindani kwa nguvu zote baada ya miaka mitano ili wananchi watuhoji tuliyoyaahidi kama tumeyatekeleza au hatujayatekeleza.


"Kila nchi hata zile zilizobobea kwenye demokrasia, unapokwisha uchaguzi unakuwa ni wakati wa kazi. Haiwezekani mkawa kila siku ni siasa, watu watalima saa ngapi?

“Kila siku ni siasa, ni vyema tukatimiza wajibu wetu tuliopewa na wananchi na watatupima kwenye hilo.


"Ni matumaini yangu kuwa Watanzania tunaowaongoza wanataka maendeleo. Iwe kwa bahati nzuri au mbaya, serikali inayoongoza ni ya Chama Cha Mapinduzi.


"Yapo tuliyoyaahidi kuyatekeleza kwa wananchi katika kipindi cha miaka mitano, nisingependa kuona mtu yeyote ananichelewesha kutekeleza hayo niliyoahidi kwa kipindi cha miaka mitano," alisema.


Alisema ushindani ambao unatakiwa ufanywe kwa nguvu ni kwa wale wawakilishi waliopewa mamlaka na wananchi kupeleka hoja zao kwenye maeneo yao.


"Kama ni madiwani, wakapeleke hoja kwa nguvu zote kwenye maeneo yao, kama ni wabunge wakazungumze kwa nguvu sana bungeni, lakini hata kuziba midomo nayo ni demokrasia, hiyo ni demokrasia ya mwelekeo wa aina yake," Rais Magufuli alisema.

Habari Kubwa