Polepole sasa aanza vita rasmi na Ukawa

25Jan 2017
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Polepole sasa aanza vita rasmi na Ukawa

KATIBU wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole, sasa ni dhahiri ameanzisha 'vita' rasmi na Ukawa, baada ya jana kubainisha kuwa chama hicho tawala kimeona kitashinda uchaguzi mkuu ujao.

Humphrey Polepole.

Hatua hiyo ya Polepole inatokana na viongozi kadhaa wakuu wa upinzani wakiwa tayari wameshatabiri kifo cha CCM kabla ya mwaka 2020.

Vyama vya siasa vinavyounda Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi) ni NCCR Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na NLD ambavyo kwa pamoja viliamua kumuunga mkono Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kuwania urais kupitia Chadema katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015.

Licha ya kushindwa na Rais John Magufuli katika uchaguzi mkuu uliopita, Lowassa bado hajakata tamaa na juzi alikaririwa akisema njia ya kuingia Ikulu 2020 ni nyeupe kwa upinzani.

Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Chadema aliyasema hayo Kahama, kijiji cha Mseki nyumbani kwa Kada wa Chadema, James Lambeli.

Alisema anashindwa kuzungumza na wananchi wa kijiji hicho kwa kuhofia kukamatwa na polisi kama alivyofanyiwa Geita na kuwataka wananchi kuwa wavumilivu mpaka itakapofika 2020.

Wakati Lowassa akitoa tambo hizo, Polepole aliibuka jana kuzijibu akieleza kuwa CCM imeanza kuona mwanga mpya na mkubwa wa kung`ara kwake kuelekea mwaka 2020, mwaka wa uchaguzi mkuu mwingine.

Polepole alisema kung'ara kwa CCM kipindi hiki ni salamu kwa baadhi ya viongozi wa vyama vingine vya siasa wanaokitabiria kifo chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu uchaguzi mdogo uliofanyika Jumapili, Polepole alisema uchaguzi huo umeonyesha mwanga wa chama hicho kukubalika zaidi.

Alisema tayari chama hicho kimeanza kuzaliwa upya kwa kuweka viongozi waadilifu, wanyenyekevu na wenye kuakisi matatizo na matarajio ya Watanzania.

Polepole pia alisema mwaka huu wa uchaguzi ndani ya chama hicho ambao alitamba CCM itazaliwa upya kwa kuwa wamelenga kupata viongozi bora.

Alisema katika mitandao mbalimbali ya kijamii kumekuwapo na mijadala kwamba huenda CCM mpaka mwaka 2020 itakuwa imekufa, lakini akatamba kuwa upo mwaka wa chama hicho kung'ara zaidi.

"Nizungumzie kazi yetu kuelekea mwaka 2020, kwa sababu wako baadhi ya viongozi wa vyama vingine ambao siyo wa CCM, wamekuwa wakitoa kauli kwamba tukutane mwaka 2020, na sisi tumeshaahidi tutafanya siasa safi inayojikita katika siasa ya maendeleo,” alisema.

“Kama kuna watu walikuwa wametutabiria giza mwaka mwaka 2020, sisi kupitia Watanzania na kwa sauti hii kubwa katika uchaguzi mdogo wamezungumza yenye ushindi wa zaidi ya asilimia 90 kwa idadi ya kata zilizoshiriki kwenye uchaguzi huo uliofanyika juzi (Jumapili).

"Kwetu (CCM) tunauona mwanga mkubwa na unatupa hamasa ya kutenda zaidi na zaidi kuwaletea Watanzania maendeleo," alifafanua zaidi Polepole pasi na kumtaja kiongozi yeyote wa upinzani ingawa kauli yake ilionyesha dhahiri kumlenga Lowassa aliyetamba ushindi upo Chadema mwaka 2020.

CCM MPYA
Polepole alisema mwelekeo wa chama hicho ni kuwa na CCM mpya yenye mageuzi ambayo ndiyo chachu ya kuipata Tanzania mpya na kwamba mwaka huu wote utakuwa ni kwa ajili ya kuzaliwa upya kwa chama hicho.

“Tutakuwa na uchaguzi ndani ya chama mwaka huu, sote tuwalipe Watanzania kwa matokeo haya makubwa waliyotupa katika uchaguzi kwa kuwapatia viongozi bora katika ngazi za uchaguzi wa CCM, waaminifu, wachapakazi, waadilifu, wanyenyekevu ambao wako tayari kuwahudumia Watanzania, wanaochukizwa na rushwa," alisema Polepole.

"Mwaka 2020 tunauona mwanga mkubwa."

Alisema katika mwelekeo wa CCM mpya, mageuzi makubwa ya kiuongozi ambayo chama hicho kimelenga kuyafanya yana lengo la kuhakikisha wanakuwa na viongozi ambao wanaakisi matarajio na mahitaji ya Watanzania.

Alisema wanataka wawe na viongozi hao waadilifu, waaminifu wachapa kazi, wanaochukia rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma, wawajibikaji, wanyenyekevu na wanaofanya kazi kwa sababu wameamini wana mchango katika kuwaletea maisha mazuri na maendeleo Watanzania.

Polepole alisema matokeo ya uchaguzi mdogo yamewapa nguvu kubwa ya kusonga mbele huku akiwapiga kijembe CUF kwa kudai kuwa wamekumbwa na anguko kubwa. Nipashe haijathibitisha anguko hilo, hata hivyo.

“Katika takwimu za 2015, jimbo la Dimani kulinganisha na matokeo ya kura ya CUF, zimeshuka zaidi kwa zaidi ya asilimia 50, wakati za CCM zimeongezeka, kwa hiyo kushindwa kwa CUF na kupungua kwa kura kwa kiasi kikubwa Dimani lazima kuna mchawi ndani yao wenyewe, wamtafute, hasa kule kule Zanzibar.

"Sisi (CCM) tumetoa taarifa kwa nia njema tu kwamba kama sisi tunavyoweka mambo yetu vizuri ndani ya chama chetu wao pia wanatakiwa kuweka mambo yao vizuri," alisema.

Polepole alisema siri ya ushindi wa CCM katika uchaguzi huo ni kuzaliwa upya kwa chama hicho na kwamba mageuzi makubwa hayo yanalenga kurejesha chama kwa wanachama na kushughulika na shida za wananchi.

Alisema Watanzania wamepokipokea chama hicho kurejea katika misingi ambayo kwayo ndiyo chama hicho kilianzishwa.

Alidai siri ya pili ni kazi nzuri inayofanywa na serikali ya chama hicho katika kushughulikia kero za wananchi hususani kupambana na masuala ya rushwa na ufisadi, na ambayo tayari imekwisha chukua hatua mbalimbali kwa watuhumiwa ikiwamo kutoa huduma mbalimbali za kiuchumi na suala la elimu bure.

MATATIZO YA WANANCHI
Alisema katika kuhakikisha chama hicho kinapata mafanikio makubwa mwaka 2020, tayari kimeelekeza kila mteule wa chama hicho kuhakikisha anatenga muda wake wa kusikiliza matatizo ya wananchi na kuyafanyia kazi.

Mbali na kumjibu Lowassa, maelezo ya Polepole pia yanaonekana kujibu salamu za Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo juzi ambapo alisema hayana uhusiano wa moja kwa moja na hasi na "matokeo yetu ya Uchaguzi Mkuu unaofuatia".

"On the contrary (badala yake), uchaguzi wa marudio unatupa fursa ya kupanda mbegu ambayo, ikitunzwa vizuri, inakuwa na mazao bora kwenye chaguzi zinazofuatia.

"Tutathmini kazi tuliyoifanya na matokeo tuliyoyapata. Tupate mafundisho sahihi ya kazi hiyo na matokeo yake. Tutumie mafundisho hayo kwa kujipanga vizuri zaidi kwa ajili ya ‘the real prize’ (kombe lenyewe): 2020."

Aidha, viongozi wengine wa upinzani kama Mwenyekiti wa Kamati ya Mpito ya Chama cha Wananchi (CUF) na hata Katibu Mkuu wake, Maalim Seif Shariff Hamad, wamewahi kuitabiria CCM anguko.

Habari Kubwa