Polisi 152 wafukuzwa kazi

08Nov 2016
Na Mwandishi Wetu
DODOMA
Nipashe
Polisi 152 wafukuzwa kazi

JUMLA ya askari wa Jeshi la Polisi 152 wamefukuzwa kazi mwaka huu kwa kukiuka sheria, taratibu na kanuni za jeshi hilo.

Hatua hiyo imetokana na kukiuka mambo yaliyoainishwa katika Kanuni za Kudumu za Polisi (PGO) namba 103.

Uamuzi huo ulitangazwa jana mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Maryam Msabaha, aliyetaka kufahamu juu ya idadi ya askari waliochukuliwa hatua kwa sababu ya utovu wa nidhamu.

Masauni alisema kuwa kazi ya vikosi vya ulinzi na usalama ni kulinda raia, mali zao pamoja na mipaka ya nchi, lakini kuna baadhi ya askari hao wanakwenda kinyume cha sheria kwa kuwapiga wananchi na kuwasababishia ulemavu pamoja na vifo, hivyo jeshi hilo limewachukulia hatua za kinidhamu.

“Jeshi la Polisi hufanya kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo, lakini kuna baadhi ya askari wamekuwa wakikiuka maadili na mwenendo mwema wa jeshi letu, hivyo kuanzia Januari 2015 hadi Juni 2016 tuliwachukulia hatua za kinidhamu askari 200,” alisema Masauni.

Naibu Waziri huyo alifafanua kuwa baada ya askari hao kuchukuliwa hatua za kinidhamu, walifanyiwa uchunguzi wa kina na jumla ya askari 152 kati ya 200 walikutwa na hatia, hivyo hatua iliyofuata ni kuwafukuza kazi.

Akizungumzia kuhusu mpango wa Serikali juu ya kujenga nyumba za askari polisi, Masauni alisema kuwa wanatambua tatizo la makazi ya askari polisi katika maeneo mbalimbali nchini hususani kwenye mikoa mipya, hivyo Serikali ina nia ya kutatua tatizo hilo kwa kuanza ujenzi wa nyumba kwa ajili ya askari hao.

“Serikali imedhamiria kupunguza tatizo la upungufu wa makazi ya askari polisi kwa kujenga nyumba kwa awamu kupitia mpango wa ujenzi wa nyumba 4,136 nchi nzima ambao utaanza kutekelezwa baada ya taratibu za mkopo wa kuwezesha ujenzi huu kukamilika,” aliongeza Masauni.

Habari Kubwa