Polisi 54 wafukuzwa kazi kwa rushwa, ujambazi

16Jul 2019
Renatus Masuguliko
GEITA
Nipashe
Polisi 54 wafukuzwa kazi kwa rushwa, ujambazi

RAIS John Magufuli amepongeza utendaji mzuri wa Jeshi la Polisi nchini, huku akieleza kuchukizwa na askari wake wachache wasio waadilifu.

Rais Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini IGP Simon Sirro wakati akitoka kukagua moja ya nyumba za makazi ya Askari wa Jeshi la Polisi katika eneo la Magogo mkoani Geita.

Amebainisha kuwa katika kipindi cha miezi sita iliyopita, askari polisi 157 wamechukuliwa hatua kwa kukiuka taratibu za kiutumishi. Kati yao, 54 wamefukuzwa jeshini.

Rais Magufuli aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa nyumba 20 za askari polisi zilizojengwa kwenye Mtaa wa Magogo mjini Geita.

Kutokana na kuwapo kwa changamoto hiyo, Rais Magufuli alimtaka Mkuu wa Jeshi la Polisi nchni (IGP), Simon Sirro, kuwa mkali kwa wanaokiuka maadili na kuchafua sifa nzuri za jeshi hilo.

Akifafanua zaidi kuhusu changamoto hiyo, Rais Magufuli alisema baadhi ya askari hao wamewajibishwa kutokana na makosa mbalimbali yakiwamo vitendo vya kushiriki katika kutenda uhalifu ukiwamo ujambazi na rushwa.

Alimtaka IGP Sirro kutokubali wachache walioko katika jeshi hilo, kuchafua heshima na sifa ya jeshi hilo ambalo yeye analiamini na wananchi wanalikubali kwa utendaji wake mzuri.

''Ninapongeza kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Polisi kwani vitendo vya uhalifu ukiwamo ujambazi, hata mkoani Geita, vimepungua sana kama ambavyo pia wananchi wana imani na Jeshi la Polisi kwa uadilifu na utendaji wake," alisema.

"Kuna askari wachache tu ambao wamekuwa wakichafua sifa na heshima ya jeshi, hao wasipewe nafasi. Sirro washughulikiwe hao wachache," Rais Magufuli aliagiza.

Alisema wapo baadhi ya askari polisi wasio waadilifu, wanashirikiana na majambazi kufanya uhalifu, kubambikiza kesi wananchi wasio na makosa.

Alisema askari wa aina hiyo lazima washughulikiwe ili kutochafua taswira ya Jeshi la Polisi na kulishusha hadhi mbele ya umma.

Mradi wa ujenzi wa nyumba 400 za askari ulianza Aprili 7 jijini Arusha wakati wa maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha Rais wa kwanza wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.

Katika maadhimisho hayo, Rais Magufuli alitoa Sh. bilioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za makazi ya askari polisi, mradi ambao ulianza kutekelezwa baada ya fedha hizo kutolewa.

Kabla ya uzinduzi huo wa nyumba 20 jana, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola na IGP Sirro walimweleza Rais Magufuli kuwa askari kutoishi kambini ni changamoto inayoweza kukwamisha utekelezaji wa shughuli za kila siku za jeshi hilo.