Polisi atoweka kazini madai kumpa ujauzito mwanafunzi

15Jun 2019
Ibrahim Yassin
MBEYA
Nipashe
Polisi atoweka kazini madai kumpa ujauzito mwanafunzi

ASKARI polisi, Konstabo Daniel Mlanda wa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya, ametoroka kituo chake cha kazi baada ya kutuhumiwa kumbaka na kumpa ujauzito mwanafunzi wa kidato cha kwanza mwenye umri wa miaka 14.

MKUU WA JESHI LA POLISI NCHINI IGP SIMON SIRRO.

Mwanafunzi wa kidato cha kwanza (jina na shule vinahifadhiwa) amedai amekuwa akibakwa na askari huyo akiwa katika lindo kwa shinikizo la mama yake mlezi ambaye alikuwa na urafiki na askari huyo.

Said Juma Mohammed, mjomba wa mwanafunzi huyo, alisema juzi kuwa walipoona mwanafunzi huyo anakuwa mvivu wa kwenda shuleni, alianza kufuatilia mwenendo wake na kubaini kuwa na uhusiano na askari huyo.

Alisema baada ya kufuatilia na kumhoji, alikiri kuwa na uhusiano wa kimapenzi na askari huyo na pia alimweleza kuwa ana ujauzito.

Aisha Mohammed mama mzazi wa mwanafunzi huyo, alisema walipopata taarifa za ujauzito wa mwanafunzi huyo, walianza kumhoji na kumtaja askari huyo kuwa ndiye mhusika baada ya kumwingilia kimwili kinguvu pasipo ridhaa yake.

“Mtoto huyu baada ya kuzidi kumhoji, alisema mara ya kwanza aliingiliwa kinguvu na askari huyo na baadaye alimgeuza kama mkewe na kumsababishia ujauzito licha ya kuwa ni mwanafunzi,” alisema.

Baada ya taarifa hizo kuvuja, imeelezwa kuwa vikao vya siri vilianza kufanyika ili kuficha tukio hilo licha ya wananchi kutaka hatua za kisheria zichukuliwe.

William Singo, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Bondeni ‘A’, alipotakiwa kuzungumzia sakata hilo baada ya kudaiwa kuficha siri, alikanusha kuhusika na vikao vinavyodaiwa kufanyika.

Mkurugenzi wa Kituo cha Msaada wa Kisheria Wilaya ya Kyela, Anna Minga.  ni miongoni mwa watu walioeleza kukerwa na tukio hilo, ambaye alisema baada ya kupata taarifa, alianza kufuatilia lakini askari huyo alikimbilia kusikojulikana.

Mbali ya tukio hilo, Mlanda pia anahusishwa na tukio lingine la kumpa mimba binti mwingine Prisca Minga (19) na kumzalisha mtoto wa kiume mwenye umri wa miezi mitano.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Sebastian Mbuta, amethibitisha tuhuma dhidi ya askari huyo  na kwamba wanalifanyia kazi suala hilo.

Habari Kubwa