Polisi: Disko toto marufuku Idd Dar

20Jul 2021
Maulid Mmbaga
Dar es Salaam
Nipashe
Polisi: Disko toto marufuku Idd Dar

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limepiga marufuku ‘Disko toto’ katika kumbi zote za starehe, katika kipindi cha kusherehekea sikukuu ya Eid Al Adha inayotarajiwa kuadhimishwa kesho.

Sikukuu ya Eid Al Adha huadhimishwa kila mwaka duniani na waumini wa dini ya Kiislamu na huadhimishwa kuanzia siku 10 tangu kuonekana kwa mwezi wa Dhu al-Hijjah kwa mujibu wa imani ya dini hiyo.

Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Muliro Jumanne, alisema Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama limejipanga kikamilifu kuimarisha usalama katika kipindi hicho.

Pia aliwaasa wananchi wa eneo hilo na Watanzania kwa ujumla kusherehekea sikukuu hiyo kwa amani na utulivu, sambamba na kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa sheria.

“Jeshi la Polisi Kanda Maalum limejipanga kuimarisha doria maeneo yote muhimu zikiwamo nyumba za ibada, fukwe za bahari na kumbi za starehe na maeneo mengine yote yatakayokuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu ili kuhakikisha wananchi wote wanasherehekea sikukuu hii kwa amani na utulivu.

“Pia wamiliki wa kumbi za starehe wanatakiwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa kumbi hizo,” alisema Muliro.

Aliongeza kwa kuwataka wazazi kuhakikisha kuwa watoto wao hawatembei peke yao bila ya kuwa na uangalizi wa karibu na kutowaruhusu kuogelea peke yao ili wasizame na kupoteza maisha.

Aidha, madereva wa vyombo vya moto waendelee kufuata sheria za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kutoendesha magari au pikipiki wakiwa wametumia pombe/vilezi.
 

Habari Kubwa