Polisi, JukeCUF wavutana kuhusu maandamano Dar

24Feb 2016
Mary Geofrey
Dar
Nipashe
Polisi, JukeCUF wavutana kuhusu maandamano Dar

JUMUIYA ya Wanawake wa Chama Cha Wananchi (JukeCUF) na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, wameendelea kuvutana juu ya maandamano ya amani yaliyokuwa yamepangwa kufanywa jana na jumuiya hiyo.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dra es Salaam, Simon Sirro.

Wiki iliyopita, jumuiya hiyo ilipanga kufanya maandamano ya amani ya kuunga mkono maazimio ya kikao cha Baraza Kuu Taifa, kutoshiriki marudio ya uchaguzi wa Zanzibar uliopangwa kufanyika Machi 20, mwaka huu, lakini Jeshi la Polisi liliyazuia.

Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Saverena Mwijage, jana alilieleza Nipashe kuwa, Kamanda wa Polisi kanda hiyo, Simon Sirro, aliwaeleza sababu za kuzuia maandamano hayo kuwa uchaguzi huo umetangazwa kufanyika Zanzibar kwa maana ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) na si Tanzania Bara.

Alisema sababu nyingine ni kuhatarisha usalama wa raia na mali zao kutokana na siku waliyoomba kufanya maandamano ni ya kazi.

Alisema pia waliambiwa waandike barua ya kuomba kibali cha kumuona Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ili kumueleza walichokusudia.

“Barua hiyo tulijibiwa Ijumaa wiki iliyopita siku moja baada ya kupeleka barua ya kuomba kibali na hata hivyo, hatukuridhishwa kabisa na sababu za kuzuia maandamano yetu kwani tunalenga kufanya kwa amani,” alisema.

Mwijage alisema kutokana na Zec kuendelea kutoa msimamo wake wa marudio ya uchaguzi na kudai barua aliyoandika aliyekuwa mgombea wao, Maalim Seif Sharif Hamad, kuwa siyo halali na hajajiondoa kwenye uchaguzi huo, walilazimika kuandika barua nyingine ya kuomba maandamano jana.

“Kwa sababu Zec bado wanaendelea na msimamo wao wa kurudia kwa uchaguzi na kumlazimisha mgombea wetu kuwa ni halali wakati alishaandika barua na sisi tunapinga vikali na dunia itambue jambo hili batili, kupitia maandamano haya ya amani,” alisisitiza.

Alisema jana waliandika tena barua na kuituma kwa Jeshi la Polisi kuomba kibali cha kufanya maandamano ya amani.

“Kwa sababu walishasema maandamano yetu tuliomba siku ya kazi, basi tumeomba watupangie siku ambayo tutayafanya bila kubughudhi watu,” alisema.

Maandamano hayo yalipangwa kuanzia katika Makao Makuu ya CUF Buguruni na kupita barabara ya Uhuru, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Karume, Kariakoo, Mnazi Mmoja, Central Polisi, barabara ya Sokoine, Bandarini, Mahakama Kuu na Ardhi hadi Ofisi ya Makamu wa Rais.