Polisi lawamani kifo cha mtoto

07Nov 2019
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Polisi lawamani kifo cha mtoto

WANANCHI wa Kijiji cha Mkunywa katika Kata ya Madibira wilayani Mbarali, Mkoa wa Mbeya, wamelituhumu Jeshi la Polisi kusababisha kifo cha mtoto, Jidamabi Lwenge (15), ambaye anadaiwa kufa maji alipotumbukia mtoni wakati akifukuzwa na askari.

Wananchi wa kijiji cha Mkunywa katika Kata ya Madibira wilayani Mbarali, wakiufunika mwili wa mtoto, Jidamabi Lwenge (15), baada ya kuuopoa kutoka katika Mto Lyandembela, Jumatatu Novemba 4, ambamo anadaiwa kutumbukia wakati alipokuwa anafukuzwa na askari wa Jeshi la Polisi, waliomtuhumu kuchungia mifugo kwenye mashamba ya chama cha ushirika wa wakulima wa mpunga Madibira. PICHA: NEBART MSOKWA

Askari hao walikuwa wanamtuhumu kuchungia mifugo kwenye mashamba ya Chama cha Ushirika wa Wakulima wa Mpunga wa Madibila (Mamcos).

Wakizungumza na waandishi wa habari kijijini hapo, wananchi hao walidai kuwa Lwenge pamoja na mwenzake mmoja walikuwa walienda eneo hilo kwa ajili ya kunywesha mifugo ndipo wakaanza kufukuzwa na askari hao ambao walikuwa wamebeba silaha za moto.

Mmoja wa wananchi hao, Mwigulu Ucheyeki, alisema mtoto mmoja ambaye alifanikiwa kuwatoroka askari hao, alienda kutoa taarifa nyumbani kwamba mifugo imekamatwa, lakini walipomuuliza kuhusu mwenzake aliko, alisema hajui alikoelekea.

Alisema baada ya kupewa taarifa hizo, alienda Polisi kwa ajili ya kukomboa mifugo, na alipofika alitozwa faini ya Sh. 2,000,000 na akarejea nayo nyumbani, lakini walipojaribu kumtafuta Lwenge, hakuonekana.

“Mchungaji wangu alinieleza kuwa walitishiwa na bunduki kisha wakaanza kukimbia kila mtu uelekeo wake, ikabidi tumuulize maeneo walipokuwa, na ndipo tukamkuta Lwenge siku ya pili mwili wake ukiwa unaning’inia hapa akiwa ameshafariki,” alisema Ucheyeki.

Alisema wamekuwa wakinyanyaswa mara kwa mara na askari hao, ambao wanakamata mifugo hata kama haipo kwenye mashamba ya ushirika ili walipe faini.

Naye Daniel Limbe, alisema askari hao wanawafanya wafugaji wa Kijiji hicho kama kitega uchumi kwa kukamata mifugo yao mara kwa mara na kuwatoza faini, huku akidai kuwa wakati mwingine hawapewi stakabadhi za malipo.

Alisema kwa sasa hawana amani katika eneo hilo kutokana na manyanyaso wanayoyapata kutoka kwa askari hao, ambao huwa wanawatoza shilingi 50,000 kwa kila ng’ombe anayekamatwa na askari, na kwamba wakati mwingine huwa wanalazimisha hata kama mifugo hiyo haipo kwenye mashamba ya ushirika.

Alisema kutokana na tukio la kifo cha mtoto Jidamabi, wanaiomba serikali kuingilia kati kutatua mgogoro uliopo baina yao akidai kuwa umefikia hatua mbaya ambayo sasa imeanza kugharimu maisha yao.

“Hatujawahi kuambiwa kuwa hatutakiwi kufuga katika kijiji hiki, na wala hakuna kiongozi aliyewahi kutuelimisha kuwa tunatakiwa tuchungie sehemu fulani…sasa tunaomba serikali ituelekeze kama hatutakiwi kufuga ili tutafute njia nyingine ya kuishi,” alisema Limbe.

Katibu wa Chama cha Wafugaji wa Wilaya ya Mbarali, Matagili Mbigili, aliwataka wafugaji hao kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho wanafuatilia tatizo hilo, huku akisisitiza kuwa serikali ya awamu ya tano ni sikivu na itawasaidia.

Aliwataka wananchi hao kuendelea kushikamana hasa katika kudai haki yao, na kwamba yeye kama kiongozi atahakikisha suala hilo linaisha na wafugaji wanapata haki.

KAULI YA POLISI

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Ulrich Matei, alikana askari wake kusababisha kifo cha mtoto huyo kwa madai kuwa alikufa baada ya kuzidiwa na maji wakati akivusha mifugo.

Alisema baada ya tukio hilo, wananchi hao walitoa taarifa katika Kituo cha Polisi cha Madibira na ndipo waliposhirikiana kuutafuta mwili, na kwamba baada ya kuupata familia ilikabidhiwa kwa ajili ya kuendelea na taratibu za mazishi.

Habari Kubwa