Polisi matatani kwa tuhuma za rushwa ya mil. 30/-

10Jul 2019
Ibrahim Yassin
Mbozi
Nipashe
Polisi matatani kwa tuhuma za rushwa ya mil. 30/-

ASKARI polisi wawili wanashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa tuhuma za kuomba na kupokea rushwa ya Sh. milioni 30.

Takukuru imewataja askari hao kuwa ni Justin Madauda namba G1466 na Anthony namba H2433 wa mkoani Songwe, ambao wanadaiwa kudai kiasi hicho cha fedha kutoka kwa mtu anayedaiwa kumiliki silaha bila kuwa na kibali.

Kamanda wa Takukuru mkoani Songwe, Damas Suta, amesema askari hao ambao mmoja ni wa kituo cha Tunduma wilayani Momba mkoani Songwe na mwingine ni wa kituo cha polisi Mahenge mkoani Morogoro, ambao walimkamata mwananchi mmoja anayedhaniwa kumiliki silaha kinyume cha sheria, huku wakimuomba rushwa ili wasimkamate.

Kwa mujibu wa kamanda huyo wa Takukuru, wanatarajia kufikishwa mahakamani baada ya taratibu kikamilika.

Kamanda Sutta, amewapongeza wananchi kwa kuonesha ushirikiano wao mzuri kwa maofisa wa taasisi hiyo na kuwataka waendelee kufanya hivyo pindi watakapohitajika, na watakapoona kuna viashiria vya rushwa mahala popote.
Katika hatua nyingine, Kamanda Sutta, amesema halmashauri ya Wilaya ya Mbozi na Ileje ni miongoni mwa halmashauri ambazo viongozi ama watendaji wake baadhi yao wanaongoza kwa kupokea rushwa.

Pia amewataka watumishi hao kufanya kazi kwa kufuata misingi ya utawala bora na kwamba Halmashauri ya Mbozi pekee Takukuru imeokoa kiasi cha Sh. 51,814,100.

Habari Kubwa