Polisi, mtuhumiwa ujambazi wapambana dakika 30, auawa

28Jun 2016
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Polisi, mtuhumiwa ujambazi wapambana dakika 30, auawa

WAKAZI wa Tandika Mabatini, mtaa wa kwa Mbonde Yangumacho, wameshuhudia mapambano ya dakika 30 baina ya jeshi hilo na mtu aliyedaiwa kuwa ni jambazi na kufanikiwa kumuua.

Tukio hilo lilitokea jana, ikiwa ni siku ya tatu, tangu Rais Dk. John Magufuli alipolitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha linawanyang’anya silaha majambazi.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo, wakati wa uzinduzi wa mpango wa kuboresha usalama wa jamii kwa jeshi hilo, uliofanyika viwanja vya Biafra jijini Dar es Salaam.

Katika mapambano hayo, wanayoyafananisha na sinema, mashuhuda waliiambia Nipashe kuwa yalianza saa mbili asubuhi, huku milio ya risasi na mabomu vikisikika.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi hao walisema Jeshi la Polisi lilipiga kambi katika mtaa wao tangu juzi usiku majira ya saa tano, huku askari wake wakirandaranda kila mtaa, hali iliyowapa hofu.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Sharif Jumbe, alisema alipewa taarifa kwa kupigiwa simu na mmoja wa wakazi wake saa moja asubuhi kuwa kuna nyumba moja ina watu ambao hawafahamiki wametokea wapi.

Alisema baada ya kupokea taarifa hiyo alishtuka, hivyo kuchukua hatua ya kupiga simu kituo cha Polisi cha Tandika na kutoa taarifa.

Aliendelea kueleza kuwa mara baada ya kutoa taarifa hizo, alienda katika eneo la nyumba hiyo na kabla hajafika alikutana na gari la polisi likiwa limeegeshwa mita kadhaa kutoka katika nyumba hiyo na kwamba alifika na kujitambulisha kwa polisi hao, ambao walimweleza kuwa katika mtaa wake kuna watu ambao si salama.

Alisema polisi hao walimweleza kuwa awaarifu wananchi wake kuwa endapo wangesikia milio ya risasi, wasishtuke na wasitoke ndani ya nyumba zao.

"Nilipoambiwa hivyo nikaondoka na haikupita hata nusu saa, nikasikia milio ya risasi na mtu mmoja alifariki dunia, lakini simjui kwa kuwa alikuwa mgeni katika mtaa wangu," alisema Jumbe.

Shuhuda mwingine, Ahmed Yusuph Maalim, ambaye ni dereva bodaboda, alisema alikuwa anatoka msikitini alfajiri ya saa 11 na alipofika katika kituo chake cha kazi, aliwakuta watu watano waliokuwa wamekaa, ambao walikuwa wageni machoni mwake.

Alisema watu hao walimwuliza: "Umefuata nini eneo hili au umefuata abiria?". Naye aliwajibu: “sijafuata abiria hili ni eneo langu la kazi.”

Maalim alisema baada ya kuwajibu hivyo nao wakamwambia: “Tumemfuata mtu, akija tutatumia pikipiki yako.”
Alisema baada ya kuambiwa hivyo, aliondoka na abiria aliyempeleka katika Hospitali ya Rufani ya Temeke.

“Hata niliporudi kutoka hospitalini, nilimkuta mwenzangu kijiweni naye aliniuliza kuhusu watu hao wageni waliokuwa wamekaa kijiweni kwetu na kila mtu mtaani alikuwa anawazungumzia hao watu,” alisema Maalim.

Alisema ilipofika saa 12:30, walifika sungusungu wa mtaa katika eneo hilo ambao nao walikuwa wana wasiwasi na watu hao.

Maalim alisema watu hao waliondoka watatu na kubaki wawili na kwamba wakati huo polisi nao walikuwa wanarandaranda katika mtaa huo.

Alisema ilipofika majira ya saa mbili asubuhi, polisi hao walikuwa wanaingia na kutoka katika moja ya nyumba ziliyoko mtaani hapo, ambayo nje ilikuwa na mashine ya kusaga.

Alisema muda mfupi baadaye, alitoka kijana katika uchochoro wa nyumba hiyo akiwa amevalia kanzu nyeupe, ndipo polisi walipomwona na kisha wakamwita kijana huyo, lakini alikaidi.

Alisema baada ya kijana huyo kukaidi, polisi hao walimwamuru asimame, lakini alikaidi pia ndipo wakaanza kupiga risasi hewani.

Shuhuda huyo alisema baada ya polisi kupiga risasi hewani, kijana huyo alianza kukimbia na ndipo polisi walimpiga risasi mguuni na kudondoka chini.

“Muda wote huo, nilikuwa nimekaa pale nashuhudia sinema yote hiyo. Unaona hata pale kwenye kibanda cha Tigo Pesa kuna tundu la risasi, askari mmoja alikuwa anapiga risasi ovyo hata kiongozi wao alimfokea kwa kumwambia alenge shabaha,” alisema Maalim.

Alisema mtu huyo alikuwa amevalia kanzu na viatu vya wazi, baada ya kudondoka alikunja kanzu yake na kusujudu kisha kutoa bomu na bunduki na kuanza kupambana na polisi hao.

Maalim alisema mtu huyo aliwarushia bomu hilo askari ambao walitawanyika kabla halijawafikia na kwamba alianza kujibizana na polisi kwa bunduki lakini walifanikiwa kumuua palepale.

Farida Twaha, mkazi wa eneo hilo, alisema kijana huyo alikuwa ametoka Mkoa wa Mwanza juzi na alifikia eneo la Ukonga kabla ya jana kufika Tandika Mabatini ili aungane na wenzake kwenda kufanya tukio la uhalifu.

Asha Bakari, mkazi mwingine wa eneo hilo, alisema mbali na kuuawa kwa mtu huyo, polisi pia walifanikiwa kumkamata mmiliki wa nyumba aliyofikia kijana huyo, aliyefahamika kwa jina la Nassoro pamoja na kijana mwingine Babu Ally, ambao wote walijeruhiwa na polisi wakati wakitaka kukimbia.

KAULI YA KAMANDA SIRRO

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro, alimtaja aliyehusika na mauaji ya kuchinja Mwanza kuwa ni Salum Said (30) mkazi wa Kiseke, ambaye alikamatwa usiku wa kuamkia jana, baada ya kutegewa mtego na jeshi hilo.

Sirro alisema majambazi hayo ni watu ambao wamekuwa wakihusika na matukio makubwa katika miji hiyo na kwamba jambazi kutoka Mwanza ndilo limekuwa likihusika katika matukio ya uhalifu katika mapango na hufundisha vijana kuingia katika mtandao wake.

Alisema kufanikiwa kwa jeshi hilo kuwatia mbaroni, kulitokana na mtego ambao waliweka baada ya kupata taarifa kwamba majambazi hayo yamekimbilia Dar es Salaam.

Kamishna Sirro alisema Jeshi Polisi lilifika katika eneo hilo na kuzingira nyumba, lakini jambazi hilo lilijaribu kukimbia kwa kupitia dirishani na kulipua bomu la mkono.

Alisema kabla ya kufanya hivyo, alipigwa risasi ya mguu na wakati wanamkimbiza hospitali akafia njiani.

Imeandikwa na Gwamaka Alipipi na Elizabeth Zaya

www.guardian.co.tz/circulation

Habari Kubwa