Polisi tuhuma ubakaji asota rumande

03Nov 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Polisi tuhuma ubakaji asota rumande

ASKARI wa Ofisi ya Upelelezi Mkoa wa Temeke, Dar es Salaam, ameendelea kushikiliwa na jeshi hilo kwa tuhuma za kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka sita.

Nipashe ilizungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, Emmanuel Lukula, ambaye alisema mashitaka yake ya kijeshi yanaendelea.

“Bado tunamshikilia mahabusu mashikata ya kijeshi yanaendelea kwa hiyo adhabu yake ikitolewa anaweza kuadhibiwa kijeshi na kama atafukuzwa kazi atafikishwa mahakamani,” alisema Kamanda Lukula.

Alisema watakapokamilisha upelelezi na kubaini kuwa ni kweli amehusika, watamwajibisha kwa kumfukuza kazi kisha kumfikisha mahakamani.

Aidha, alisema yanapotokea matukio kama hayo, kuna changamoto  zinazojitokeza ikiwamo wananchi kushindwa kwenda kutoa ushahidi.

“Kama wangekuwa wamekuja kwa wakati tungekuwa tumemaliza jambo hili, sasa tatizo ni kwamba kuna shahidi mmoja ambaye ni muhimu ndiye alikuwa anakwamisha, lakini nimesikia amekuja leo (jana), hivyo watakamilisha jadala na kunipatia ili hatua zichukuliwe,” alisema Kamanda Lukula.

Tukio hilo lilitokea wiki moja iliyopita. Inadaiwa kuwa askari huyo akiwa amelewa, alimbaka mtoto huyo ambaye analelewa na bibi yake, anayeishi kwenye nyumba ambayo pia askari huyo amepanga.

Habari Kubwa