Polisi waahidi ulinzi sherehe za Mapinduzi

11Jan 2020
Peter Mkwavila
Dodoma
Nipashe
Polisi waahidi ulinzi sherehe za Mapinduzi

JESHI la Polisi limesema kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, limepanga na kuweka mikakati kuhakikisha kunakuwapo na ulinzi wa kutosha katika sikukuu ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, picha mtandao

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime, alisema kwa kutambua umuhimu wa sherehe hiyo ambayo pia ni kumbukumbu ya mapinduzi hayo, Jeshi la Polisi limejipanga kuimarisha ulinzi.

"Jeshi la Polisi tumejipanga kuhakikisha sherehe zinasherehekewa kwa amani, utulivu na usalama wa hali ya juu kabisa," Misime aliahidi.

Alisema mikoa na vikosi vyote vimepewa maelekezo na wamejipanga vizuri kuhakikisha hali ya amani inatawala kipindi chote cha sherehe hizo.

Hata hiyo, aliwataka wananchi kuwa umoja, amani, utulivu, usalama na mshikamano mkubwa katika sherehe hizo.

Alitoa wito kwa wananchi na wadau wote kuwa pamoja na kwamba Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wameimarisha ulinzi na kuwataka wanapoona tukio au jambo lolote lisilo la kawaida, kutoa taarifa haraka kwa viongozi wa polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama.

"Kama inavyofahamika Januari 12, mwaka huu, siku ya Jumapili Watanzania kwa ujumla wanasherehekea sikukuu ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Tumeimarisha ulinzi maeneo yote," alitamba.

Alisema siku hiyo ni muhimu kwa taifa kwa kuwa inakumbusha historia ya nchi.

Wakati huo, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro, amempongeza Rais John Magufuli kwa kuliwezesha jeshi hilo kuimarisha miundombinu yake mbalimbali ikiwamo mradi wa ujenzi wa nyumba 400 za makazi ya askari zilizojengwa nchi nzima.

IGP Sirro alisema jana kuwa ujenzi huo tayari umekamilika na askari wameanza kutumia nyumba hizo.

Habari Kubwa