Polisi wafanya operesheni Kibiti

05Aug 2021
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Polisi wafanya operesheni Kibiti

OPERESHENI ya siku tatu ya Jeshi la Polisi iliyofanywa katika Wilaya za Kibiti, Mkuranga na Rufiji mkoani Pwani ili kubaini shughuli zozote za kiuhalifu ikiwamo viashiria vya kigaidi, imejiridhisha maeneo hayo kwa sasa ni shwari.

Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime, katika taarifa yake aliyoitoa jana, alisema Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Kamishna Msaidizi wa Polisi Kungu Malulu, aliongoza operesheni hiyo iliyofanyika kuanzia Jumamosi iliyopita na kumalizika Jumatatu.

Aliwataka wengine walioshiriki operesheni hiyo ni maofisa, wakaguzi na askari wenye vyeo mbalimbali kutoka Dar es Salaam, Pwani na Rufiji.

“Jeshi la Polisi linaendelea kuwashukuru wananchi kwa ushirikiano wanaoendelea kutoa kwetu na kuwezesha kupata mafanikio katika kubaini, kuzuia na kupambana na uhalifu na wahalifu,” alisema.

Misime alisema wanatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano na pale watakapoona viashiria vyovyote vya kihalifu katika maeneo yao, watoe taarifa ili hatua stahiki zichukuliwe kwa wakati na kuepusha madhara.

“Jeshi la Polisi linaendelea kusisitiza umuhimu wa kila Mtanzania kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi na anayekwenda kinyume, tutamchukulia kuwa lengo lake ni kuvuruga amani na utulivu na hatutasita kumchukulia hatua stahiki kwa mujibu wa sheria,” alionya.

Alisema jeshi hilo liliamua kufanya operesheni hiyo maalum ya kukagua maeneo yaliyokuwa maficho ya wahalifu wenye kujihusisha na matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha na matukio yenye mrengo wa kigaidi.

“Kama mnavyokumbuka eneo hilo la Rufiji kuanzia mwaka 2014 hadi 2017 lilikuwa na matukio ya mauaji, unyang’anyi wa kutumia silaha na vitendo vyenye mrengo wa kigaidi.

“Kazi kubwa ilifanywa na Jeshi la Polisi katika kipindi hicho kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama na wananchi na kufanikisha kuwapata wahalifu na silaha nyingi zikiwamo za kivita,” alisema.

Aliongeza kuwa baada ya operesheni hiyo ya miaka hiyo, Jeshi la Polisi liliona umuhimu wa kufanya nyingine kukagua maeneo yaliyokuwa yanatumiwa na wahalifu kwa kipindi hicho yakiwamo ya Wilaya ya Kibiti kama Rungungu na Nyambunda.

Alisema maeneo mengine yaliyochunguzwa ni ya Mkuranga katika eneo la Bupu na Mamndimkondo na Rufiji eneo la Nyamitumba Ngomboroni na Kifuru.

Pia alisema operesheni hiyo imefanyika katika mapori yanayopatikana maeneo hayo.