Polisi walalamikia adhabu ndogo za mahakama kwa makosa barabarani

09Jan 2017
Mwinyi Sadallah
Zanzibar
Nipashe
Polisi walalamikia adhabu ndogo za mahakama kwa makosa barabarani

JESHI la Polisi Zanzibar limesema adhabu ndogo za makosa ya usalama barabarani zinazotolewa na mahakama zinachangia kuongezeka kwa ajali na watu kupoteza maisha visiwani humo.

Hayo yalisemwa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Zanzibar, Mkadam Khamis Mkadam, alipokua akitoa tathimini ya ajali za barabarani visiwani hapa baada ya kumaliza mwaka 2016.

Alisema adhabu ya Sh. 5,000 zinazotolewa na mahakama kwa makosa ya barabarani kwa vyombo vya moto ni ndogo ikilinganishwa na madhara wanayopata wananchi na wakati mwingine kupoteza maisha.

“Hata Mrajisi wa mahakama kuu tumezungumza naye adhabu wanazotoa mahakakimu kwa kesi za makosa ya usalama barabarani ni ndogo, wakosaji wanatozwa hadi faini ya Sh. 5,000, ndiyo maana watu wanarudia kufanya makosa,” alisema.

Mkadam alisema kama adhabu ingekuwa kali hakuna mtu ambaye angerudia makosa ya usalama barabarani na kutaka mamlaka husika kutunga kanuni za adhabu za papo kwa hapo kama inavyofanyika Tanzania Bara.

Alisema kwa mujibu wa sheria ya mawasiliano na usafirishaji ya Zanzibar, kanuni hizo zinatakiwa kutungwa na waziri na utekelezaji wake kusimamiwa na Jeshi la Polisi.

“Tunasubili waziri mwenye dhamana ya usafirishaji kutunga kanuni, lakini kuna haja katika utekelezaji wa adhabu za hapo kwa hapo kusimamiwa na Bodi ya Mapato Zanzibar ili kukusanya fedha kwa kushirikiana na polisi lakini hii itategemea msimamo wa serikali,”alisema Mkadam.

Alisema mwaka 2016 ajali za barabarani 562 zilitokea Zanzibar na watu 156 walipoteza maisha, wanaume wakiwa 124 na wanawake 32, wakiwamo watoto 35, wakati majeruhi walikuwa 848 katika ajali hizo.

Alisema jumla ya makosa 29,846 ya usalama barabarani yalitokea katika kipindi hicho na wahusika kufikishwa katika vyombo vya sheria, ambapo Sh. milioni 270 zilikusanywa kutokana na adhabu walizotozwa wahusika.

Hata hivyo, alisema ajali zimepunguza Zanzibar kutoka 604 mpaka 562 sawa na asilimia 6.9, lakini majeruhi wameongezeka na kufikia 849 sawa na asilimia 7 kutoka 26,164 mpaka 29,848.

Mkuu huyo wa Kikosi cha Usalama Barabarani Zanzibar alisema ajali nyingi visiwani hapa zinatokana na uzembe ikiwamo mwendo kasi, ulevi na kukosekana mfumo mmoja wa mtaala wa udereva kutokana na kuibuka kwa vyuo vingi vya udereva.

Habari Kubwa