Polisi walivyorushiana risasi majambazi saa 2

07Dec 2017
Mary Mosha
Nipashe
Polisi walivyorushiana risasi majambazi saa 2

WAHALIFU sugu watatu waliokuwa wakihusika na kesi za unyan’ganyi kwa kutumia silaha na mauaji ndani na nje ya mkoa wa Kilimanjaro kati ya mwaka 2012-2015  waliuawa juzi katika msitu wa Njoro, Manispaa ya Moshi, baada ya kurushiana risasi na polisi kwa saa mbili, imeelezwa.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Hamiss Issa

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issa  alisema jana kuwa mapigano hayo ya risasi yalitokea juzi katika msitu wa Njoro na jeshi lake kuwaua Juma Mdoe, Francis Kinyaiya na Valerian Joachim maarufu Valee.

Alisema majambazi hao ambao walikuwa wametoka kutumikia vifungo jela, walirejea mitaani na kuanza kujihusisha tena na matukio ya uhalifu.

Mapema mwezi huu, Kamanda Issa alisema, polisi walipata tetesi kuwa majambazi hayo yanakaa katika msitu huo ulio katika kata ya Njoro, hivyo jeshi hilo kuanza msako mkali kwa kushirikiana na raia wema.

Alisema baada ya kuwabaini, wahalifu hao walianza majibizano ya risasi kwa zaidi ya saa mbili dhidi ya polisi waliokuwa wamevamia msituni hapo.

Kamanda Issa alisema kumbukumbu zinaonyesha majambazi hao waliwahi kuwa wahalifu sugu ndani ya mkoa wa Kilimanjaro na ya jirani.

Alisema miongoni mwa matukio hayo ni unyang'aji  wa kutumia silaha.

Kamanda Issa alisema kumbukumbu za polisi zinaonyesha Mdoe aliwahi kuwa na kesi ya mauaji  mwaka 2015.Aidha, alisema kamanda huyo, Kinyaiya alikuwa na kesi ya mauaji ya mwaka 2013 na Valee alikuwa na kesi ya mauaji ya mwaka 2012.

Kamanda Issa alisema katika majibizano hayo, jambazi mmoja aliuawa hapo hapo na wengine wawili walifariki wakati wakikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi ambako miili yao ilihifadhiwa kwa ajili ya utambuzi.

“Askari baada ya kupata taarifa ya wahalifu hao kutoka kwa wananchi, walifuatilia na kuvamia msitu wa Njoro ili kuhakikisha wanawatia kizuizini," alisema Kamanda Isaa na kueleza zaidi:

"Lakini watuhumiwa walianza kufyatua risasi kwa askari hali ambayo ilileta majibizano ya risasi ambayo yalipelekea umauti wao.”

Alisema uchunguzi wa awali wa polisi ulibaini majambazi hayo yalihusika katika uvamizi ambao mlinzi mmoja alifungwa kamba za miguu na mikono na kuzibwa mdomo kwa matambara Novemba 24, mwaka huu.

Katika tukio hilo la maeneo ya Uru Shimbe, kamanda huyo alisema bunduki mbili aina ya shortgun ziliporwa.

“Katika eneo la tukio (mapigano ya risasi ya juzi)  kulikutwa bunduki moja aina ya shortgun Greener  iliyokatwa mtutu na ambayo namba zake zimefutwa," alisema Kamanda Issa, "risasi tatu, maganda matatu, mapanga mawili, mkasi mmoja wa kukatia makufuli, kirungu kimoja na tindo ya kutindulia milango  pamoja na bangi misokoto miwili.”

Aidha, kamanda huyo alisema marehemu hao walikuwa wakishirikiana na kundi lingine la watu ambalo lilipanga kutekeleza uhalifu hasa kuelekea kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka.

Alisema anawataka kuacha mara moja njama hizo na kuwaomba wananchi kutoa ushirikiano wa hali na mali ili kuhakikisha mkoa wa Kilimanjaro unabaki salama.

MAMIA YA WATU

Nipashe ilifika katika Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi na kukuta umati wa watu uliofika kutambua miili ya majambazi hao huku kukiwa na vilio na simanzi.

Eriki Musa, Samweli Elikana na Magdalena Lyimo ni baadhi ya wakazi wa Moshi ambao waliiambia Nipashe  kuwa wamefika katika hospitali hiyo kwa lengo la kutambua miili hiyo.

Aidha, diwani wa kata ya Njoro kwa tiketi ya Chadema, Jomba Koi, alikiri kusikia majibizano ya risasa majira ya jioni na walipofika eneo la tukio   walikuta tayari jambazi mmoja ameuawa.

Alisema wawili walikuwa mahututi.

“Ni kweli kuna tukio kama hili katika kata yangu," alisema Koi, "na mtu mmoja kati ya hao ametambulika kuwa ni mkazi wa kata ya yangu"."Hao wengine siwajui.”