Polisi wamwita aliyewatuhumu kumpora fedha

15Jun 2019
Romana Mallya
DAR
Nipashe
Polisi wamwita aliyewatuhumu kumpora fedha

JESHI la Polisi mkoani Mwanza limemwita mkazi wa Dar es Salaam, Nixon Moshi, ambaye aliwatuhumu askari watatu mkoani humo kuwa walimpora Sh. 1,188,000 akiwa huko kwa ajili ya kuhani msiba.

Juzi, Nipashe iliandika habari ya Moshi ambaye aliandika barua ya wazi kwenda kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro, na kutaka ichapishwe gazetini ili kumsaidia arudishiwe fedha zake alizodai walichukua askari hao.

Jana, alipotafutwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Jumanne Muliro, ili kujua nini kinachoendelea kuhusiana na suala hilo, ndipo alipomtaka Moshi aende Mwanza.

"Kwa sababu jalada la kesi limefunguliwa Mwanza anatakiwa aje huku. Tayari Mkuu wa Upelelezi Mkoa Mwanza (RCO ameshapewa maelekezo," alisema Kamanda Muliro.

Baada ya Nipashe kupokea barua ya Moshi, ilimpigia simu ndipo aliposema pamoja na fedha hizo, zipo zingine kiasi cha Sh. 990,000 zilizotokana na matumizi aliyofanya wakati wote akiwa mkoani humo akisubiri uchunguzi.

Katika barua yake, Moshi alidai kuwa  Mei 14, mwaka huu, akiwa mkoani humo alikwenda kwenye duka la fedha akiwa na Sh. 1,630,000 kwa ajili ya kuwekewa fedha hizo kwenye simu lakini mhudumu alimwambia kuwa ana Sh. 600,000 kwenye simu yake.

"Nilimkabidhi mhudumu wa M-Pesa Sh. 600,000 akadai bado Sh. 5,000, nilipompa kabla hajaniwekea fedha kwenye simu yangu alitoka nje ya duka na aliporudi alikuwa ameambatana na mlinzi wa benki ambaye ni JKT Suma, yule mhudumu akasema mimi ni mwizi nataka kumwibia nimempa fedha pungufu," ameandika Moshi.

Katika barua hiyo, Moshi amedai kuwa simu ilipigwa polisi na walifika askari na kumchukua kuelekea kituoni.

"Pale pale askari waliniuliza nina shilingi ngapi, nikawajibu jumla ni Sh. 1,630,000 na nikitoa nilizomkabidhi mhudumu wa M-Pesa, nilizo nazo mfukoni ni Sh. milioni 1,030,000," aliandika.

Moshi aliendelea kudai kuwa waliondoka na askari hao ambao walijitambulisha kwa majina bandia, Lyimo wakati ni Novatus, Dula wakati ni Abdalah na watatu ambaye hakujitambulisha.

"Askari hawa hawakunipeleka mapokezi ya kituo cha polisi waliniingiza kwenye vyumba ambako ni karibu na kituo cha polisi vimepakana na ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Mkoa (RCO), walinipekuwa hawakuandika PPR ili isijulikane kiasi nilichokuwa nacho.

"Walichukua maelezo na baadaye wakaniambia Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) anazitaka fedha. Wakanirudishia Sh. 442,000. Hawakunifungulia kesi yoyote wakaniambia nijidhamini kwa Sh. 500,000 ya maneno, wakaniruhusu nikaondoka."

Moshi alidai kuwa Mei 15, aliamua kuwasiliana na Kamanda wa Polisi wa mkoa huo pamoja na RCO ili wamsaidie ndipo walipomwambia aende kwa OCD.

"Nilikwenda kwa OCD na askari wale walipatikana na RCO akasema ufanyike uchunguzi na kazi hiyo alipewa askari Sajenti Christopher (ametaja namba yake ya simu), baada ya uchunguzi RCO akaamua kuwa askari hao wasirudishe fedha na akachukua simu yangu kuwa wanaifanyia uchunguzi, nilisubiri majibu kila nikipiga simu kwa Christopher akawa hapokei," ameandika.

Moshi ameandika kwenye barua hiyo kuwa kutokana na hali hiyo aliamua kurudi Dar es Salaam na ameomba vyombo husika kufuatilia ili arudishiwe fedha zake Sh. milioni 1,188,000 pamoja na alizotumia kusubiri wakati wote kiasi cha Sh. 990,000.

Nipashe ilipomtafuta Sajenti Christopher ili kujua kama anafahamu suala hilo alisema hafahamu tukio hilo wala mtu huyo na kumuomba ni vyema aende Mwanza, ili wakutane amuone.

"Yeye anasema alikuwa Mwanza akaondoka, aje Mwanza sizijui habari hizi unazoniambia kama kulikuwa na mkwamo kwa nini asirudi kwa RPC, simfahamu wala kesi siifahamu," alisema.

Habari Kubwa